Habari

Imewekwa: Dec, 15 2020

Kongwa: Huduma ya Maji Kuimarishwa

News Images

Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ameahidi kushughulikia tatizo la upatikanaji wa maji lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2020/21 mpaka 2021/22.

Mhandisi Sanga ametoa ahadi hiyo alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi kuhusu upatikanaji wa maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, jijini Dodoma.

"Tumetoa ahadi ambazo zinatekelezeka na kimsingi kazi za ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Sugutu zitaanza jumatatu hii na nimeelekeza mradi huu ujengwe ndani ya miezi miwili na katika kijiji cha Ndurugumi kutajengwa mradi wa shilingi milioni 910 ndani ya miezi hii mitatu na kazi itaanza ndani ya siku 14 ", Mhandisi Sanga amesema na kuongeza kuwa miradi hiyo itakapomalizika itanufaisha na vijiji vingine vilivyo karibu na maeneo hayo.

Aidha, Katibu Mkuu amewataka wananchi ambao maeneo yao yatapitiwa na miradi hiyo kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa mitaro.

Awali, katika ziara hiyo baadhi ya wananchi wa vijiji vya Suguta na Ndurugumi walitoa malalamiko yao juu ya changamoto za upatikanaji wa maji zinazowakabili.

Naye, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Kongwa, Mhe. Job Ndugai (Mb) amewataka wananchi kutunza miundombinu ya maji ili miradi hiyo iwe endelevu.

"Lazima wawepo vijana wetu wa kukagua usalama wa hiyo miradi ili iwe endelevu kwa sababu tuna tabia tofauti, kwa mfano mwingine anatoboa usiku ili maji yaende nyumbani kwake, mwingine anatoboa ili maji yamwagike kwenye bustani yake, wengine wanapeleka mifugo na tabia nyinginezo kama hizo ", Mhe. Ndugai amefafanua.

Ziara ya Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Wilayani Kongwa ni mwendelezo wa ziara zake za kikazi katika kusikiliza kero za wananchi kuhusu upatikanaji wa majina kuzipatia ufumbuzi. Ziara hiyo pia iliijumuisha kutembelea mradi wa uchimbaji wa visima katika kijiji cha Ibwaga na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Vihingo.

Kitengo cha Mawasiliano