Habari

Imewekwa: Jul, 24 2019

Kampuni Zatakiwa Kukamilisha Mradi wa Maji Ndani ya Miezi Miwili

News Images

TAARIFA KWA UMMA

Waziri wa Maji Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) amezitaka kampuni zinazohusika na ujenzi wa mradi wa maji wa Malinyi mkoani Morogoro kukamilisha kazi hiyo ndani ya miezi miwili kuanzia leo. Kampuni hizo niAUDACIA INVESTIMENT LTD inayohusika na ujenzi pamoja na Kampuni ya Ushauri ya INTER CONSULT LTD.

Maelekezo hayo yameambatana na makubaliano yaliyofanyika kwenye ofisi za Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) baina ya kampuni ya AUDACIA INVESTIMENT LTD, INTER CONSULT LTD na Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi wa MazingiraVijijini (RUWASA).

Katika makubaliano hayo, Kampuni ya AUDACIA INVESTIMENT LTD na INTER CONSULT LTD zitawajibika kurekebisha mradi ndani ya siku 75 na wananchi wawe wanapata majisafi na salama kwa gharama zao.

Marekebisho hayo yanayokadiriwa kufikia shilingi milioni 450 yanatokana na kukosewa kwa mradi hali iliyosababisha mradi kuchelewa kuanza kutoa huduma kwa zaidi ya miaka mitatu hadi hivi sasa. Mradi huo ambao haujakamilika unatekelezwa kwa zaidi ya shilingi bilioni tatu ambapo tayari zaidi ya shilingi bilioni 2.8 zimeshatumika.

Profesa Mbarawa (Mb) amesema kuwa Wizara ya Maji haitaingia gharama na wala haitawajibika kurekebisha mradi wa maji wowote nchini ambao hautoi huduma kwa sababu ya kukosewa na kampuni yoyote.

Ameongeza kuwa utaratibu wa kupitia upya gharama za miradi utaendelea kwa sababu amebaini miradi mingi ya maji inatekelezwa kwa gharama kubwa.

Waziri Prof. Mbarawa amewataka wakandarasi na wakandarasi washauri na wafanyakazi wa Wizara ya Maji kufanya kazi kwa weledi na kwa uaminifu mkubwa kwa manufaa ya wananchi.

Kitengo cha Mawasiliano

24 Julai, 2019