Habari

Imewekwa: Nov, 07 2021

Fainali za Maji Cup zafunguliwa Dodoma. Mbeya wawachapa Dodoma 3-0

News Images

Watanzania wametakiwa kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa miundombinu ya maji ili kuzuia upotevu wa maji. Wito huo umetolewa jana Novemba 6, 2021 na Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Utoaji wa Huduma kutoka Wizara ya Maji Mhandisi Lyidia Joseph kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhanndisi Anthony Sanga wakati akifungua fainali za mpira wa miguu za kuwania kombe la maji (Maji Cup - 2021)

Lydia amesema serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kutandaza miundombinu ya maji ili yaweze kuwafikia watanzania wengi zaidi lakini baadhi ya watu wamekuwa wakishiriki kuiba maji hayo na kuharibu miundombinu hali ambayo imekuwa ikiongeza gharama za uzalishaji maji.

“Siku zote upotevu wa maji unarudisha nyuma juhudi za serikali. Tunatumia gharama kubwa kuweka miundmbinu lakini watu wanafungua koki maji yanamwagika hovyo, wanaiba maji, hivyo kila Mtanzania popote pale alipo anapaswa kuhakikisha anashiriki katika kuzuia upotevu wa maji."

Amewashukuru waandaaji wa mashindano hayo Umoja wa Wasambazaji Maji Nchini (ATAWAS) kwa kutambua umuhimu wa michezo na kuitumia kufikisha ujumbe kwa jamii. Amesema michezo inapendwa na wengi hivyo inasaidia kuleta afya ya akili, na kusaidia utendaji wa kila siku katika kutoa huduma kwa wananchi hatimae kusaidia kuondoa changamoto zinazoikumba sekta ya maji nchini.

Kwa upande wake mwakilishi wa shirikisho la soka nchini TFF Osca Milambo pamoja na mwakishi kutoka Wizara ya Sanaa Utamaduni na Michezo wameishukuru ATAWAS na Wizara ya Maji kwa kutambua umuhimu wa michezo na kuitumia kufikisha ujumbe wa kuzuia upotevu wa maji.

Fainali za Maji Cup zinafanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ambapo timu za Sekta ya maji kutoka sehemu mbalimbali nchini zinashiriki katika mashindano hayo ambayo yanalenga kuhamasisha uzuiaji wa upotevu wa maji. Katika mchezo wa ufunguzi uliofanyika jana timu ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya( Mbeya UWSA) imeifunga timu ya Mamlaka ya maji Dodoma (DUWASA) goli tatu kwa moja.