Habari

Imewekwa: Jan, 11 2023

​Aweso awakabidhi RUWASA magari mapya . Aagiza kazi iendelee

News Images

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Hamidu Aweso (Mb) amemkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Wakalawa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Clement Kivegalo magari 10 yaliyogharimu Sh bilioni 1.5. ili yatumike katika shughuli za Wakala huo sehemu mbalimbali mikoani.

Hafla ya makabidhiano ya magari hayo imefanyika katika ofisi za Rasimali za Maji jijini Dodoma na kuhudhuriwa na baadhi ya watumishi wa Wizara hiyo.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi magari hayo Mhe. Aweso amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa nia yake ya dhati ya kuhakikisha changamoto za watumishi katika Wizara ya Maji zinapatiwa ufumbuzi. Pia amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa wakala huo kuhakikisha magari hayo yanatumika kufanikisha ufuatiliaji wa miradi na sio kinyume na hapo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji RUWASA Mhandisi Clement Kivegalo amesema uhitaji wa magari kwa ajili ya Wakala huo ni magari 398 nchi nzima na magari yaliyopo ni 392 ambayo hata hivyo hayana ubora sana kwani ni ya muda mrefu. Kutokana na uhitaji huo serikali imekuwa ikijitahidi kuhakikisha magari mapya yananunuliwa ili kurahisisha shughuli vya ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi ya maji vijijini.

Mpaka sasa Kibari cha kununua magari 123 kimetolewa ambapo magari 38 yameshanunuliwa na kusambazwa mikoani na yaliyokabidhiwa leo ni sehemu ya magari 25 ambayo pia yamenunuliwa kwa awamu nyingine na yote yatasambazwa sehemu mbalimbali mikoani ili kuhakikisha kazi ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani inaendelea.