Habari

Imewekwa: Jan, 07 2021

AWESO ATOA MWEZI MMOJA WANANCHI WA SHIRATI WAPATE MAJI

News Images

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (MB) ametoa siku 30 kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) kuhakikisha wananchi wa Mji wa Shirati wanapata huduma ya maji.

Ametoa maelekezo hayo Januari 6, 2021 Wilayani Rorya alipotembelea miradi ya maji wilayani hapo akiwa ameambatana na Mbunge wa Jimbo la Rorya Mhe. Jafari Chege na Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Mhe. Simon Odunga ili kujionea hali halisi sambamba na kuzungumza na wanufaika.

Ilielezwa kuwa mradi wa maji Shirati ulisimama kutoa huduma yamaji tangu mwaka 2016 baada ya mtambo wa kusukuma maji kuharibika na kwamba hadi hivi sasa hakuna hatua iliyochukuliwa.

Hata hivyo, Waziri Aweso alibainisha kwamba alikwishatoa maelekezo kwa MUWASA kufanya tathmini ya gharama zinazohitajika ili mradi huo uanze kazi.

Aidha, Mhe. Waziri alihoji kiasi cha fedha kilichopo kwenye akaunti ya Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilayani Rorya na kujibiwa kuwa akaunti hiyo inazo shilingi milioni 290 ambazo ameagiza zitumike kukamilisha mradi huo ambao gharama inayotakiwa ili uanze kutoa huduma ni shilingi milioni 247.

“Inashangaza sana unayo fedha kwenye akaunti halafu watoto wanalala njaa hii haijakaa sawa hata kidogo; wananchi hapa kipindi chote hiki wanateseka hawana maji halafu fedha ipo tu benki imekaa haitumiki kama ilivyokusudiwa,”Waziri Aweso alisema.

Mhe. Waziri akiwa hapohapo kwenye eneo la mradi alimpigia simu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga na kukubaliana fedha zilizopo kwenye akaunti ya RUWASA Rorya zitumike kutekeleza mradi wa Shirati.

Waziri Aweso alisisitiza MUWASA kukamilisha mradi kwa kipindi walichokubaliana na alisema hatokubali kisingizio chochote hasa ikizingatiwa fedha yote inayohitajika itatoka.

Aliwakumbusha watendaji kwenye Sekta ya Maji kuepuka kuzoea shida za wananchi badala yake wajikite kuwatatulia kero ya maji na alibainisha kwamba kutokana na changamoto alizozishuhudia wilayani humo amejiridhisha kwamba Meneja wa RUWASA Rorya hana uwezo wa kutosha kutatua changamoto zilizopo.

Waziri Aweso alielekeza meneja huyo apatiwe majukumu mengine na kwamba apelekwe mtaalam mwingine atakayekuwa na uwezo wa kutatua changamoto zilizopo wilayani hapo.