Habari

Imewekwa: Jan, 06 2021

Aweso Ataka Mabadiliko RUWASA Mkoa wa Mara

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amemtaka Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga kutengua uteuzi wa Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Mara, Mhandisi Sadick Chakka na Meneja wa Wilaya ya Tarime Mhandisi Marwa Murasa kwa kushindwa kusimamia vyema utekelezaji wa miradi ya maji.

Waziri alitoa kauli hiyo alipofanya ziara ya kukagua mradi wa maji wa Magoto ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Mara.

Waziri Aweso alisema lengo la kuanzisha RUWASA ni kuhakikisha wananchi wanapata maji na maelekezo ya awali ni kuwa kabla utekelezaji wa miradi haujaanza kila Meneja wa RUWASA Mkoa alipaswa kuwasilisha taarifa ya kuanisha miradi yenye kero kwa wananchi (miradi kichefuchefu) lakini RUWASA Mkoa wa Mara haikufanya hivyo.

“Haiwezekani mradi upo asilimia 98 na hautoi maji, unawezaje kujenga tenki hali ya kuwa huna uhakika kama maji yapo? Ulipaswa kujiridhisha na chanzo chako kwanza ili kuhakikisha maji yapo ya kutosha na hatua zingine zinafuata,” Waziri Aweso alihoji.

Aidha, mara baada ya kutembelea mradi huo na kujionea hali halisi sambamba na kuzungumza na wananchi wa maeneo hayo, Waziri Aweso alijiridhisha na kubaini kwamba mradi huo haujatekelezwa kama inavyopaswa.

“Bora hata kisingizio kingekuwa uhaba wa fedha kama ambavyo hua mnadanganya lakini kwa mkoa wa Mara tumeleta ziadi ya shilingi bilioni nane na fedha iliyopo kwenye akaunti hadi sasa ni zaidi ya shilingi bilioni 3 hivi ni nani atakuelewa wakati wananchi hawana maji na kwenye akaunti una fedha ya kutosha,” Waziri Aweso alihoji.

Aliongeza kuwa taarifa ya utekelezaji wa miradi wilayani humo inasikitisha kwani tathmini inaonesha miradi mingi imekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 lakini haitoi maji na hivyo aliwataka wataalam kote nchini kutumia vyema utaalamu wao badala ya kujiamulia kujenga miradi kiholela.

Aidha, Waziri Aweso amemtaka Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga kujiridhisha na uwezo wa wataalam na watendaji wa RUWASA na kuhakikisha wale wasiokuwa na uwezo wanaondolewa.

Naye, Mbunge wa Tarime vijijini na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Mwita Waitara (Mb) ambaye aliambatana na Waziri Aweso katika ziara hiyo alisema hali ya upatikanaji wa majisafi na salama kwa wananchi wa Tarime hairidhishi.

Waziri Aweso yupo mkoani Mara kwa ziara ya kikazi kukagua miradi ya maji hususan inayotekelezwa maeneo ya vijijini.

Kitengo cha Mawasiliano