Habari

Imewekwa: Jan, 07 2021

AWESO AMUAGIZA DC RORYA KUMSAKA MKANDARASI ALIYETEKELEZA MRADI WA MAJI KIROGO

News Images

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Mhe. Simon Odunga kumtafuta mkandarasi aliyehusika na ujenzi wa mradi wa maji wa Kirogo wilayani humo.

Ametoa agizo hilo Januari 6, 2021 alipofanya ziara ya kukagua mradi na kujiridhisha kuwa mkandarasi wake alillipwa shilingi bilioni 1 ambayo ni sawa na asilimia 98 ya mkataba wake licha ya kwamba mradi huo haujakamilika.

“Kwa nini mkandarasi amelipwa fedha yote yaani asilimia 98 haliyakuwa mradi haujakamilika,” alihoji Waziri Aweso

Alisema inawezekana wakandarasi waliokuwa wakipewa kazi za ujenzi wa miradi wilayani humo hawakuangaliwa uwezo wao wa utekelezaji wa miradi na badala yake wamekuwa wakipewa kazi kiujamaa na alitahadharisha kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watakaobainika kupeana kazi kwa namna hiyo.

Waziri Aweso alikagua mradi huo wenye vituo 27 vya kuchotea maji kwa ajili ya vijiji vya Kirogo, Wamaya na Nyabiwe na kukuta vituo vichache vikifanya kazi, huku vituo vingi vikiwa havitoi maji bila kuwepo sababu ya msingi wala maelezo yanayojitosheleza jambo ambalo lilimkera.

Alielekeza wasimamizi wa miradi ya maji kote nchini (wilayani na mikoani) kuhakikisha wanashirikiana na viongozi wa Serikali kwenye maeneo yao na pia wahakikishe wanawasilisha taarifa za miradi kwenye vyombo vya maamuzi ikiwemo baraza la madiwani juu ya shughuli wanazoendelea nazo na alisisitiza kwamba mhandisi atakeyekaidi wizara itamchukulia hatua.

Vilevile, ameelekeza Wiki ya Maji mwezi Machi iwe ni maalum kwa jili ya uzinduzi wa miradi.

“Tarehe 22 Machi, Wiki ya maji hatutaki iwe ya porojo na mapambio, tunataka iwe ya uzinduzi wa miradi, tunataka wiki ya maji iwe ni ya Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kutoa zawadi ya miradi ya maji kwa wananchi wake,” alielekeza Waziri Aweso.

Mara baada ya ziara za ukaguzi wa miradi, Waziri Aweso alikutana na watumishi wote wa Sekta ya Maji Mkoani Mara kujadili changamoto zinazokwamisha shughuli za kuwafikishia wananchi huduma ya maji.