Habari

Imewekwa: Jul, 16 2019

RUWASA Kuwa Mwarobaini wa Changamoto za Maji Vijijini

News Images

TAARIFA KWA UMMA

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ndio mwarobaini wa changamoto za miradi ya maji inayotekelezwa maeneo ya vijijini hapa nchini.

Mhe. Aweso (Mb) amesema hayo wakati akifungua kikao kazi kuhusu uendeshaji wa RUWASA kilichofanyika jijini Dodoma na kusisitiza wote watakaohusika katika kuharibu miradi ya maji watachukuliwa hatua.

Naibu Waziri Aweso amesema lengo ni kuinua kiwango cha Sekta ya Maji kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya maji katika maeneo ya vijijini. Ameitaka RUWASA kuhakikisha inatatua changamoto za muda mrefu za maji vijijini kwa kufuatilia na kusimamia vizuri miradi yote ya maji, inayoendelea na iliyokamilika.

Amewataka wahandisi na wataalam wote katika Sekta ya Maji nchini kufanya kazi zinazowahusu ili kupata tija kwenye uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali kwenye miradi ya maji.

Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo akiongea katika kikao hicho amesema kuanzishwa kwa RUWASA ni namna bora ya mfumo wa uendeshaji wa Sekta ya Maji nchini na kuwataka wataalam wote waliopata nafasi na wale ambao hawakupata kushirikiana pamoja katika kuhakikisha lengo la kufikisha maji kwa wananchi linatimia.

Prof. Mkumbo amesema Mameneja wa Wilaya wa RUWASA nchini watawajibika moja kwa moja na miradi ya maji inayotekelezwa katika maeneo yao na hawatakiwi kuwa na sababu yoyote kutotekeleza wajibu wao ipasavyo, hivyo wanatakiwa kuelewa majukumu yao kwa ufasaha.

Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) imeanza kazi tarehe 1 Julai, 2019 kupitia Sheria Na. 5 ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira ya Mwaka 2019.

Kitengo cha Mawasiliano

16 Julai, 2019