Habari

Imewekwa: Jan, 15 2020

Naibu Waziri Maji Awataka Wataalam Kuachana na Michakato

News Images

Simiyu; 06 Januari, 2020

TAARIFA KWA UMMA

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewataka wataalam wa Sekta ya Maji nchini kuachana na michakato isiyo na ulazima kwa kuwa imekuwa ikikwamisha Serikali katika utekelezaji wake wa miradi ya maji.

Maelekezo hayo yametokana na Mhe. Aweso kukuta utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maji mkoani Simiyu imechelewa kutokana mchakato wa manunuzi unaochukua muda mrefu kukamilika na mingine ikisubiri kibali kutoka RUWASA makao makuu jambo ambalo halikumfurahisha Naibu Waziri Aweso.

“Niwaombe wataalam wetu wote kwenye Sekta ya Maji tuache michakato isiyo na ulazima katika hatua zote kuanzia upembuzi yakinifu mpaka hatua ya mwisho ya kuanza ujenzi wa miradi jambo hili linatuchelewesha sana, tufanye vitendo’’, ameelekeza Naibu Waziri Aweso.

“Kwa Mkoa wa Simiyu pekee Mamlaka ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ina Shilingi bilioni 6.9 kwa ajili ya miradi ya maji, wakati Wilaya ya Bariadi pekee ina Shilingi bilioni 1.3 tatizo ni michakato mirefu, niwaombe sana tuachane na tabia hii na tufanye kazi”, ameonya Mhe. Aweso.

Pia, akatolea mfano mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda kwenye wilaya za Bariadi, Busega, Itilima, Maswa na Meatu mkoani Simiyu ambao uthamini wake haujakamilika na kusababisha utekelezaji wake kuchelewa.

“Serikali ya Awamu ya Tano siyo serikali ya michakato ni serikali ya vitendo, lakini pia kipimo cha RUWASA ni maji bombani na si maneno kwa sababu fedha zipo za kutosha’’, amesisitiza Naibu Waziri Aweso.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Aweso amemuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Maji kumchukulia hatua za kinidhamu Mhandisi Conrad Mkomoya kwenda kinyume na utaratibu wa kazi kwenye ujenzi wa Mradi wa Maji wa Igaganulwa ulioanza mwaka 2012 na kiasi cha Shilingi milioni 726 kimeshatolewa lakini bado haujakamilika katika Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu.

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini