Wasifu

Prof. Kitila Mkumbo

Katibu Mkuu

Prof. Kitila Mkumbo

Prof. Kitila Alexander Mkumbo aliteuliwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji tarehe 4 Aprili 2017, na kuapishwa rasmi kushika wadhifa huu tarehe 5 Aprili 2017. Kabla ya uteuzi huu, Prof. Mkumbo alifanya kazi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwanza kama Afisa Tawala kuanzia mwaka 1999 hadi 2003 ambapo baada ya hapo alijiunga na kada ya taaluma. Prof. Mkumbo alipanda katika ngazi mbalimbali za kitaaluma kutoka Mhadhiri Msaidizi mwaka 2003 hadi kuwa Profesa Mshiriki mwaka 2014.

Akiwa mwanataaluma na moja ya wasomi wa jamii wanaojulikana ndani na nje ya Tanzania, Prof. Mkumbo amechapisha makala nyingi katika majarida ya kitaaluma. Aidha, Prof. Mkumbo amefanya kazi nyingi za ushauri wa kitaaluma kwa mashirika mbalimbali ya kimataifa na kitaifa, pamoja na Serikali.

Prof. Kitila Alexander Mkumbo ana Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Southampton, nchini Uingereza, na Shahada ya Uzamili katika Saikolojia ya Jamii kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Prof. Mkumbo pia ana Shahada ya Kwanza katika Sayansi na Elimu (BSc. Ed.) akiwa amesomea kufundisha masomo ya Baiolojia na Kemia.

Prof. Mkumbo alizaliwa tarehe 21 Juni 1971, na alisoma elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Mgela, Wilaya ya Iramba Mkoani Singida kati ya mwaka 1981 na 1987, na Elimu ya Sekondari katika Shule ya Sekondari Mwenge Mkoani Singida kati ya mwaka 1988 na 1991. Prof. Mkumbo alisoma Elimu ya Juu ya Sekondari katika Shule ya Sekondari Pugu, Jijini Dar es Salaam.