Taarifa kwa Umma

HOTUBA YA WAZIRI WA MAJI MHE. PROF. MAKAME MBARAWA (MB) WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO KATI YA WIZARA YA MAJI NA MAMLAKA ZA MAJISAFI NA USAFI WA MAZINGIRA MIJINI PAMOJA NA WATAALAM WA MAJI WA MIKOA KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WA HAZINA JIJINI DODOMA - TAREHE 7 NOVEMBA, 2018

Mhe. Jumaa Aweso, Naibu Waziri wa Maji,

Prof. Kitila Mkumbo, Katibu Mkuu Wizara ya Maji,

Mhandisi Emmanuel Kalobelo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji,

Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),

Wakurugenzi na Wataalamu kutoka Wizara ya Maji,

Wataalamu wa Maji wa Mikoa (RS)

Watendaji Wakuu wa Taasisi na Wakala zilizo chini ya Wizara,

Watendaji Wakuu wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira (Mikoa, Wilaya, Miji Midogo na Miradi ya Kitaifa),

Wageni Waalikwa,

Wana Habari,

Mabibi na Mabwana.

Ndugu Washiriki,

Awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kutujalia sisi sote afya njema na kutuwezesha kuhudhuria katika Mkutano huu muhimu. Ninamshukuru Menejimenti ya Wizara kwa kufanikisha jukumu la kutukutanisha ili kujadili masuala mbalimbali kuhusiana na hali ya huduma ya maji nchini. Ninawashukuru pia, washiriki wote mliopo hapa kwa kukubali wito na kuhudhuria Mkutano huu. Ninaamini katika mkutano huu wa siku mbili tutajadiliana na kukubaliana mambo ya msingi katika kusukuma mbele zaidi utoaji wa huduma ya maji hapa nchini.

Ndugu Washiriki,

Nichukue nafasi hii kuwashukuru viongozi na watumishi wote katika sekta ya maji nchini kwa kazi kubwa wanayofanya katika kuhakikisha kuwa nchi yetu inaondokana na tatizo kubwa la upatikanaji wa huduma ya maji. Ninajua bado ni kubwa lakini pia kazi kubwa imeshafanyika na inaendelea kufanyika.

Ndugu Washiriki,

Maji ni hitaji muhimu sana katika uhai wa mwanadamu na viumbe wengine. Maji hayana mbadala na ndiyo maana tunasema “bila maji hakuna uhai”. Pamoja na umuhimu huo, ni ukweli usiopingika kuwa “maji ni uchumi”. Maendeleo ya kiuchumi ya nchi yoyote duniani; yawe ya viwanda, kilimo na kadhalika yanategemea maji.

Kwa kutambua umuhimu huo wa maji, Chama Cha Mapinduzi kupitia Ilani yake ya Uchaguzi ya 2015-2020 kimebainisha lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi ifikapo mwaka 2020 kufikia asilimia 85 kwa wananchi waishio vijijini na asilimia 95 kwa wananchi waishio mijini. Wajibu wa kuitekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2015-2020 na kutimiza malengo yake imepewa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Daktari John Pombe Magufuli. Ndiyo maana nimefarijika sana kukutana pamoja nanyi leo ili kujadili kwa kina namna bora itakayotuwezesha kufikia malengo yaliyobainishwa kwenye Ilani.

Ndugu Washiriki,

Nimekuwa nikizunguka nchi nzima kwa kuwatembelea katika Mamlaka zenu nikiangalia juu ya uendeshaji na utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi wanaowazunguka. Katika ziara zangu nimekuwa nikijionea changamoto mbalimbali zinazokabili utoaji wa huduma ya majisafi na uondoaji wa majitaka. Hivyo, mkutano huu wa pamoja natarajia utakuwa chachu ya kuboresha utoaji wa huduma ya majisafi na uondoaji wa majitaka kwa kila mmoja wetu pale atakaporudi katika Mamlaka yake. Kama ilivyoelezwa katika utambulisho hapa kuna Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji za Miji Mikuu ya Mikoa, Mameneja wa Mamlaka za Maji za Wilaya na Miji Midogo na Miradi ya Kitaifa pamoja na Wataalam wa Maji wa Mikoa. Ninyi ndio wahusika katika uendeshaji na utoaji wa huduma kwa wananchi wanaowazunguka. Nitumie Mkutano huu kuwaelekeza watendaji wote mambo ambayo nataka tuyajadili na mengine ni maagizo kutokana na uzoefu nilioupata kwenye ziara zangu katika baadhi ya Mamlaka za Maji nchini.

Ndugu Washiriki,

Mkutano huu ni wa kikazi hivyo pamoja na majadiliano mengine ni lazima tujadili mambo yafuatayo:

a) Hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika miji na mikakati ya kupanua huduma ya maji kuelekea mwaka 2020;

b) Mapendekezo ya viashiria vipya vya kupima utendaji wa Mamlaka (Key performance Indicators - KPI);

c) Tafsiri ya eneo la huduma kwa Mamlaka za Maji mijini;

d) Hatua iliyofikiwa katika kutunga Sheria mpya ya maji; na

e) Mapendekezo ya muundo wa RUWA na nafasi ya Mamlaka za maji katika utekelezaji wake.

Nimeona ni vyema tukayajadili haya ili kuwa na uelewa wa pamoja. Tuna changamoto nyingi katika utoaji wa huduma ya maji nchini, hivyo ninyi ni sehemu ya watatuzi wa changamoto hizo.

Ndugu Washiriki,

Pamoja na agenda mtakazojadili katika mkutano huu, nitumie nafasi kuwaelekeza yafuatayo:

1. Gharama za Umeme na Madawa ya kutibu maji kwa Mamlaka za Maji

Ndugu Washiriki, kumekuwepo na baadhi ya Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kushindwa kujilipia ankara za umeme na madawa ya kutibu maji. Mamlaka hizo endapo zitaimarisha utendaji wake zinaweza kugharamia sehemu au gharama zote za umeme na madawa. Ni vyema Mamlaka hizo zikaimarisha utendaji wake na hivyo ukusanyaji wa mapato ukaongezeka na kutumia mapato hayo katika kugharamia umeme na madawa.

2. Uwekezaji katika miradi ya maji nchini

Ndugu Washiriki, kumekuwa na utaratibu wa Mamlaka za Maji kufanya kazi kama idara za Serikali. Mamlaka hizo zimekuwa zikiitegemea Wizara kugharamia utekelezaji wa miradi midogo midogo ambayo inaweza kutekelezwa na mamlaka hizo. Nataka mtambue kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maji na mamlaka zenu ziendelee kutekeleza miradi midogo midogo kwa kupitia mapato yenu ya ndani. Aidha Mamlaka za Miji Mikuu ya Mikoa ziendelee kushiriki katika usimamizi wa miradi inayotekelezwa na Mamlaka za Miji ya Wilaya, Miji Midogo, Miradi ya Kitaifa na Halmashauri. Natambua kuwa kuna MoU inayoelekeza kuhusu kiwango cha mapato ya Mamlaka kinachotakiwa kutumika katika uwekezaji wa miradi ya maji. Mamlaka ziendelee kutekeleza makubaliano hayo.

3. Mwongozo wa matumizi ya madawa ya kutibu maji na gharama za umeme katika miradi ya maji nchini

Ndugu Washiriki, kumekuwepo na matumizi ya kiwango tofauti cha madawa ya kutibu maji katika miradi mbalimbali. Hali hiyo imepelekea kutokujulikana kwa kiwango halisi kinachotakiwa katika kutibu maji ya kiasi fulani kwa Mamlaka za Maji nchini. Naelekeza Wizara kuandaa Muongozo utakaobainisha aina, kiwango, na muda wa kutumia madawa ya kutibu maji pamoja na kiasi cha maji kinachotakiwa kutibiwa. Vile vile, kuwepo na log book ya kutunza kumbukumbu za gharama za madawa ya kutibu maji pamoja na ankara za umeme unaotumiwa kwenye miradi ya maji.

4. Bei za matumizi ya maji kwa wananchi

Ndugu Washiriki, nimebaini uwepo wa tofauti kubwa katika bei za maji kwa wananchi hasa wale wanaotumia vituo vya kuchotea maji (DPs) na wale waliounganishwa majumbani. Wananchi wanaotumia vituo vya kuchotea maji wamekuwa wakitozwa kati ya Shilingi 50 hadi 500 kwa ndoo sawa na (Shilingi 1,000 hadi 10,000 kwa mita moja ya ujazo) wakati kwa wananchi waliounganishwa majumbani ni kati ya Shilingi 300 (Geita) hadi 1,600 (DAWASA) kwa mita moja ya ujazo. hali hii haikubaliki. Naagiza EWURA pamoja na vingezo vingine wanavyotumia katika upangaji wa bei za maji pia, wazingatie kupanga bei za maji kulingana na aina ya nishati inayotumika kwa miradi mbalimbali (Solar Power, diseli na Umeme).

5. Wananchi walio karibu na vyanzo vya maji kupatiwa huduma ya maji

Ndugu Washiriki, katika ziara zangu mikoani, nimebaini kuwa baadhi ya wananchi wanaoishi karibu na vyanzo vya maji hawapati maji wakati wao ndio walinzi wa miundombinu ya maji pale walipo. Hili nalo halikubaliki. Hivyo, naagiza wananchi wote walio karibu na vyanzo vya maji wapewe kipaumbele katika kupata huduma ya maji, kwa kufanya hivyo itasaidia katika kuimarisha ulinzi wa vyanzo pamoja na miundombinu ya maji na kufanya huduma ya maji kuwa endelevu.

6. Ufuatiliajiwa miradi ya maji nchini

Ndugu Washiriki, Kumekuwa na changamoto kubwa katika ufuatiliaji wa miradi kutokana na uhaba wa fedha na mfumo wa usimamizikwa kiasi kikubwa ambapo Wizara ya Maji ilikuwa na jukumu la kupeleka fedha za miradi kwenye Halmashauri wakati usimamizi ukiwa chini ya Halmashauri, hata hivyo Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuliona hilo imeamua sekta ya maji kwa ujumla wake isimamiwe na Wizara ya Maji, ambapo tayari Wizara imeshatayarisha sheria mpya ya maji na inatarajiwa kusomwa kwa mara ya kwanza katika bunge hili linaloendelea. Hata hivyo bado tunahitaji kuongeza umakini katika ufuatiliaji wa miradi.

7. Usimamizi wa Wakandarasi na Watalaam Washauri

Ndugu Washiriki, kumekuwepo na desturi ya kuwapatia kazi wakandarasi na wataalam washauri wakati tayari wana kazi wanazoendelea kuzikamilisha na ziko katika hatua za awali. Hali hiyo inasababisha ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi ya maji. Naagiza kuwa Mkandarasi aliye na mradi zaidi ya mmoja na utekelezaji wa miradi hiyo upo chini ya asilimia 50 asipewe kazi nyingine hadi akamilishe miradi ya awali.

8. Upatikanaji wa vibali kwa wataalam kutoka nje ya nchi

Ndugu Washiriki, kumekuwepo na ucheleweshaji mkubwa wa upatikanaji wa vibali vya kufanya kazi kwa Wataalam watokao nje ya nchi wanaotekeleza miradi ya maji hapa nchini. Hali hiyo imekuwa ikisababisha ucheleweshaji wa miradi ya maji katika maeneo mbalimbali. Naagiza Wizara kuimarisha ufuatiliaji wa vibali vya Wataalam kutoka nje na kuhakiki Wataalam hao ni wale ambao sifa zao za kazi hazipatikani hapa nchini. Hali hiyo itasaidia kuharakisha utekelezaji wa miradi.

9. Viashiria vya Kupima Utendaji wa Mamlaka za Maji (KPI)

Ndugu Washiriki, nimekuwa nikipitia ripoti ya utendaji wa mamlaka za maji inayoandaliwa na EWURA kila mwaka. Katika ripoti hiyo nimebaini baadhi ya mamlaka za maji utendaji wake umekuwa ukishuka mwaka hadi mwaka. Kutokana na hali hiyo, Wizara inaandaa vigezo na viashiria vipya vya kupima ufanisi wa Watendaji wa Mamlaka. Katibu Mkuu atawasilisha rasimu ya awali ya vigezo na viashiria hivyo. Baada ya kuidhinishwa vigezo na viashiria hivyo vitatumika kila mwaka katika kupima ufanisi wa Watendaji wa Mamlaka.

10. Upotevu wa Maji (NRW)

Ndugu Washiriki, kumekuwepo na upotevu mkubwa wa maji yanayozalishwa kutokana na uchakavu wa miundombinu iliyojengwa miaka mingi iliyopita, wizi wa maji kwa wateja wasiokuwa waaminifu, kujipatia huduma ya maji kinyume na taratibu (by pass and illegal connection) pamoja na udanganyifu wa wateja kwa kuchezea dira za maji ili zisitoe taarifa sahihi za matumizi ya maji. Hali hiyo imesababisha mamlaka nyingi za maji kushindwa kujiendesha. Naagiza Mamlaka zote za maji nchini ziwe na Mkakati unaotekelezeka wa kuhakikisha upotevu wa maji nchini unapungua na kufikia kiwango cha kimataifa kilichokubaliwa ambacho ni asilimia 20.

Ndugu Washiriki,

Nimalizie hotuba yangu fupi kwa kuwashukuru tena kwa kuja kwenu hapa na ni matumaini yangu kuwa washiriki wote mtazingatia maagizo niliyoyatoa na kuyatekeleza ipasavyo, aidha mtapata nafasi ya kuchangia kikamilifu katika mada zitakazowasilishwa katika kikao kazi hiki na mtatoa mapendekezo yatakayoboresha utoaji wa huduma kwa wananchi tunaowahudumia. Baada ya kusema hayo, sasa ninatamka kuwa Mkutano Umefunguliwa Rasmi.

Ahsanteni Sana kwa Kunisikiliza na Ninawatakia Majadiliano Mema.