Habari

Imewekwa: Mar, 18 2019

Wiki ya Maji 2019: Serikali kukamilisha miradi ya maji

News Images

Wakati maadhimisho ya Wiki ya Maji yanafanyika Duniani,Serikali imejipanga kukamilisha miradi ya maji ili wananchi wapate huduma ya majisafi na salama ndani ya umbali wa mita 400 katika makazi yao.

Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Prof. Kitila Mkumbo akiongea kwa niaba ya Waziri wa Maji wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kisayansi kuhusu Sekta ya Maji nchini amesema mkakati ni kufikisha huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijijini. Kiwango hicho kimepangwa kufikiwa ifikapo mwaka 2020 ambapo takribani miradi 1600 imekamilishwa na mingine zaidi ya 400 inaendelea ili kutimiza lengo hilo kwa wananchi.

Prof. Mkumbo amesema mpaka hivi sasa ipo miji ambayo huduma ya maji inapatikana kwa asilimia 100 kama Moshi, na mingine ni chini ya kiwango hicho, mfano Arusha ipo asilimia 40 na Dar es salaam asilimia 80. Hata hivyo, hadi mwezi Februari 2019 wastani wa upatikanaji maji mjini ulikua kati ya asilimia 78 hadi 80.

Katibu Mkuu Prof. Mkumbo amesema kwa upande wa vijijini vituo vya maji 85,000 vinafanya kazi kwa kuhudumia idadi ya wananchi wapatao milioni 25, na kufanya wastani wa upatikanaji maji kuwa asilimia 64. Amesema ili kuharakisha upatikanaji wa majisafi kwa wananchi, mabadiliko yamefanyika ikiwamo kuanzisha Wakala ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

Amesema Kongamano la Kisayansi kuhusu sekta ya Maji nchini ni moja ya matukio ya Wiki ya Maji Kitaifa. Matukio mengine ni Mkutanowa Mapitio ya Sekta ya Maji (Joint Water Sector Review); na Siku ya maalum yaMamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA Day) ambapo Ripoti ya utendaji wa mamlaka za maji ya mwaka 2017/2018 itazinduliwa na kujadiliwa. Kazi nyingine zinazofanyika ni pamoja na kuzindua miradi ya maji iliyokamilika.

Mwaka 1993 Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mazingira na Maendeleo lilipitisha Azimio rasmi la kuadhimisha Siku ya Maji Duniani kila mwaka ifikapo tarehe 22 Machi.

Wizara ya Majiimekua ikiratibu na kuadhimisha siku hii muhimu kuanzia mwaka 1988. Haya yamefanyika kwa kuwashirikisha wananchi na wadau wa maji. Lengo kuu likiwa kuungana na Mataifa mengine Duniani katika kutathmini utekelezaji, mafanikio, changamoto na kuainisha mikakati ya kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira na kusimamia utunzaji wa rasilimali za maji.

Kaulimbiu ya maadhimisho haya ni ; “Hakuna Atakayeachwa: Kuongeza Kasi ya Upatikanaji wa Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa Wote katika dunia inayobadilika kitabia nchi”

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

18.03.2019