Habari

Imewekwa: Mar, 30 2019

Waziri wa Maji Aagiza Mkandarasi kurejea kazini kuendelea na kazi ya Mradi wa Tindingoma-Momba, Tunduma

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) amemtaka mkandarasi anayejenga mradi wa maji wa Tindingoma uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Momba –Tunduma katika mkoa wa Songwe kurejea na kuendelea na ujenzi wa mradi.

Waziri Mbarawa aliyasema hayo alipokuwa akikagua mradi wa maji wa Tindingoma unaotekelezwa na Mkandarasi Dacady Investmnt Co. Limited ya Dar es Salaam.

“Niliagiza madai yake kiasi cha Tsh. 143,190,793/= yasifanyike mpaka nifike katika mradi huu ili kuona kazi iliyokwisha fanyika. Kwa kuwa sasa nimeona maendeleo ya utekelezaji wa kazi hii ni mzuri na nimejiridhisha, hivyo Wizara itamlipa pesa hizo mara moja na wiki ijayo arejee kazini kuendelea na kazi ya kukamilisha mradi ili wananchi wa Momba wapate majisafi na salama”, alisema Profesa Mbarawa.

Mpaka sasa ujenzi wa miundombinu wa mradi huu umefikia asilimia 46 baada ya kujenga tanki moja lenye nguzo yenye urefu wa mita 10 na ujazo wa lita 45,000, ambalo limeshakamilika, vituo tisa vya kuchotea maji, nyumba ya pampu, kuchimba na kulaza mabomba yenye urefu wa mita 400 ambavyo baada ya kupata malipo hayo anatakiwa avikamilishe mara moja.

Aidha, Profesa Mbarawa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Momba Bw. Juma Said Irando kuita watu wa TAKUKURU kuja kufanya uchunguzi kuhusu utaratibu uliotumika kumpata Mkandarasi mpya baada ya Halmashauri ya Momba kuvunja mkataba wa Mkandarasi wa awali ajulikanaye kwa jina la Fally Enterprises Limited ya Sumbawanga.

Mkataba wa Mkandarasi huyo ulivunjwa baada ya kutoonekana katika eneo la mradi kwa kipindi cha siku 28 na licha ya kuandikiwa barua kadhaa za kumtaka kuwepo katika eneo la kazi kwa mujibu wa mkataba baada ya kutotekeleza maelekezo aliyokuwa akipewa kwenye barua alizoandikiwa. Halmashauri ilivunja mkataba tarehe 08 Mei, 2018.