Habari

Imewekwa: May, 10 2019

Watumishi Wizara ya Maji Waaswa Kuzingatia Weledi katika Utendaji Wao wa Kazi

News Images

Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo amewaasa watumishi wa Wizara ya Maji kuzingatia weledi katika utendaji wao wa kazi ili kutatua changamoto mbalimbali katika kuwafikishia wananchi huduma ya maji.

Amesema hayo wakati wa kikao na watumishi wote wa wizara kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Hazina, jijini Dodoma.

Profesa Mkumbo amesema watumishi wa kada zote wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa ufanisi kwa kuwa kila mmoja ana mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya sekta ya maji nchini.

''Kila mtumishi ni bora na mchango wake unathaminiwa. Rai yangu kwenu ni kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na kuwa waaminifu katika majukumu ya kila siku'', Profesa Mkumbo amesema.

''Jukumu letu viongozi ni kuhakikisha mnafanya kazi katika mazingira mazuri na rafiki ili muweze kutekeleza majukumu yenu kikamilifu'', Profesa Mkumbo amesisitiza.

Aidha, Profesa Mkumbo amewashukuru watumishi wote kwa utekelezaji wa kazi kwa mwaka 2018-2019 na kushiriki kikamilifu katika mpango wa mwaka 2019-2020.