Habari

Imewekwa: May, 28 2019

Wananchi Wilayani Mpimbwe Waishukuru Serikali kwa Kutimiza Ahadi ya Maji

News Images

TAARIFA KWA UMMA

Wakazi wa Kijiji cha Kijiji cha Kashishi kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, mkoani Katavi wameishukuru Serikali kwa kutimiza ahadi ya kuwapatia huduma ya majisafi na salama haraka na kumaliza tatizo la miaka mingi na kusababisha wananchi hao kutumia muda mwingi kutafuta maji baada ya kufanya kazi za uzalishaji.

Wananchi hao wametoa kauli hiyo mbele ya Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) alipokuwa kijijini hapo kuona utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa kwa wananchi hao mwishoni mwa mwaka jana, alipotembelea kijiji hicho na kukutana na malalamiko mengi kuhusu tatizo sugu la maji la muda mrefu.

Waziri wa Maji, Profesa Mbarawa amewashukuru wananchi hao kwa uvumilivu wao na kuwataka wawe walinzi wa miundombinu na kuutunza vizuri mradi huo uweze kutoa huduma kwa muda mrefu. Akisisitiza Serikali kuendelea kuwekeza fedha zaidi kwenye miradi mingine ili huduma hiyo iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi katika Wilaya ya Mpimbwe, mkoani Katavi.

‘‘Ni wajibu wetu kama Wizara ya Maji kumaliza tatizo la maji kwa wananchi, tumepanga kufikia lengo hilo kwa kufuatilia utekelezaji ya miradi yote nchi nzima kwa ukaribu. Bila kutoa nafasi kwa mkandarasi yeyote kutukwamisha, niwaambie ukweli tutawachukulia hatua na hatutakuwa na mchezo katika jambo hili’’, Profesa Mbarawa ameonya.

Akizungumza mbele ya Waziri wa Maji, Bi. Elizabeth Jonathan amesema wanawake wa kijiji walikuwa ni waathirika wakubwa wa tatizo la maji kutokana na kutembea mwendo mrefu kutafuta maji siku nzima, huku wakiacha kufanya kazi nyingine na kuziacha familia zao. Akisisitiza mradi huo mkubwa umeleta faraja kubwa kijijini hapo.

Ujenzi wa Mradi wa Maji wa Kashishi ulianza mwezi Februari, 2018 na kukamilika mwezi Aprili, 2019 ukihusisha kazi za ujenzi wa tenki la ujazo wa lita 100,000, vituo 9 vya kuchotea maji, ulazaji wa mtandao wa mabomba wenye urefu wa mita 12,500 na nyinginezo.

Mradi huo unahudumia wananchi wapatao 5,230 umegharimu zaidi ya Shilingi milioni 500 na kazi ya ujenzi imefanywa na Mkandarasi Dan General Construction Co. Ltd.

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Mei 26, 2019