Habari

Imewekwa: Mar, 23 2019

Tuongeze Kasi na Ubunifu katika Sekta ya Maji

News Images

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa (Mb) amewetaka wafanyakazi wa wizara ya maji kuongeza ubunifu, kasi ya utendaji na ufuatiliaji ili kufikia malengo ya kuwapatia wananchi huduma ya maji safi na salama, na yenye kutosheleza mapema zaidi kwa sababu huduma hiyo wanaisubiri kwa hamu.

Prof. Mbarawa amesema hayo katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Maji kilichofanyika katika ukumbi wa wizara, jijini Dodoma ambapo amesisitiza usimamizi na ufuatiliaji wa kazi ni moja ya nyenzo za mafanikio katika utendaji.

Ameongeza kuwa wataalam katika sekta ya maji wanapojitoa kwa nguvu zote katika kazi, wanaleta furaha kubwa kwa wananchi, akitolea mfano wa Mradi wa Maji wa Longido ulioanzia mto Simba mkoani Kilimanjaro ambapo, tarehe 22 Machi, 2019 wananchi walimpigia simu kuwa wanapata majisafi na salama kupitia mradi huo.

Waziri Mbarawa amesema anataka kuona kasi ya utendaji wa masuala mbalimbali katika sekta ya maji kila wakati ili kukamilisha kazi kwa wakati. Aidha, ameainisha kuwa maamuzi yanapofanyika yafanyike kwa ukweli, uwazi, uadilifu na yasiegemee upande wowote. Amewataka wale wanaotoa ushauri kwa viongozi wafanye hivyo kwa kuwa huduma ya maji ni moja ya kazi yenye heshima katika jamii yoyote.

Prof. Mbarawa ambaye kashiriki mkutano wa Baraza la Watumishi wa Wizara anayoiongoza kwa mara ya kwanza toka alipoteuliwa amewaambia watumishi yamefanyika mabadiliko ya kimfumo katika wizara kwa nia njema ya kuleta tija na ufanisi zaidi ambapo baadhi ya idara zimeunganishwa.

Mabadiliko mengine ni pamoja na kuanzishwa kwa Wakala ya Huduma za Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) na wataalam wa maji nchini kuwajibika wizara ya maji moja kwa moja. Aidha, wizara kuandaa Muongozo wa Vyama vya Watumia Maji ili kuweza kuwahudumia wananchi vizuri.

Kwa mujibu wa Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma Na. 19 ya Mwaka 2013 kabla Bajeti za wizara hazijawasilishwa Bungeni zinatakiwa kujadiliwa na kupitishwa na Mabaraza ya Wafanyakazi wa wizara husika.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano

23.03.2019