Habari

Imewekwa: May, 03 2019

Serikali Yasaini Mkataba wa Utekelezaji wa Mradi Wa Maji Simiyu (Simiyu Climate Resilience Project)

News Images

Serikali ya Tanzania na Shirika la Mazingira la Green Climate Fund (GCF) wamesaini mkataba wa msaada utakaofanikisha utekelezaji wa mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika usambazaji wa majisafi na salama katika Wilaya za Bariadi, Itilima, Meatu, Busega na Maswa mkoani Simiyu.

Kupitia mradi wa maji wakazi wapatao 300,000 watanufaika na huduma ya majisafi na salama. Aidha, mkataba huo pia unahusisha maeneo ya kilimo cha umwagiliaji katika wilaya hizo, usafi wa mazingira na kuzijengea uwezo taasisi zitakazoendesha huduma hizo, zikiwemo mamlaka za maji katika maeneo husika.

Mradi huu utagharimu jumla ya Euro mililioni 171 (Shilingi bilioni 444,600,000,000) ambazo zitachangiwa na GCF (Euro milioni 102.7), Serikali ya Tanzania (Euro milioni 43.3) na Serikali ya Ujerumani (Euro milioni 25). Katika mikataba mitatu iliyosainiwa inahusisha mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la GCF kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) wa kiasi cha Euro 102.7, mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ujerumani kupitia KfW wa kiasi cha Euro milioni 25 na mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na KfW unaohusisha utekelezaji wa mradi huo. Mradi huu utatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano tangu siku ya kusainiwa kwa mkataba huo.

Serikali imelishukuru Shirika la GCF na Serikali ya Ujerumani kwa msaada wa kiasi cha Euro milioni 127.7 (Shilingi bilioni 330) zitakazoboresha maisha ya wakazi wa Mkoa wa Simiyu katika sekta za maji, umwagiliaji na mazingira.