Habari

Imewekwa: Feb, 13 2019

Naibu Waziri Aweso Awataka Wataalamu wa Sekta ya Maji Kutumia Utaalamu wao Kutatua Kero za Wananchi

News Images

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amewataka wataalamu wote wa Sekta ya Maji nchini kutumia taaluma zao vizuri kwa kutatua kero za wananchi, jambo litakalomaliza malalamiko ya mara kwa mara.

Ametoa rai hiyo wakati akiwa wilayani Kilolo kukagua miradi ya maji ya Kilolo mjini, Ilula-Mgombezi na Ruaha Mbuyuni na kukuta malalamiko kutoka kwa wananchi yanayotokana na kutoridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo.

Naibu Waziri Aweso amesikitishwa na hali hiyo mara baada ya kugundua makosa ya kitaalamu kwenye mradi wa Ilula, ambapo umetanguliwa na ujenzi wa tenki la maji baada ya chanzo cha maji kulingana na utaratibu wa ujenzi wa miradi ya maji.

"Nitoe rai yangu kwa waatalamu wetu wote wa Sekta ya Maji kutatua kero za wananchi maana zimekuwa ni nyingi wakati wana uwezo unaotokana na elimu walizonazo, vinginevyo utaalamu wao hauna manufaa kwa taifa" amesema Naibu Waziri Aweso.

"Hakuna sababu ya wananchi kuendelea kulalamika wakati sekta ina wataalamu wa kutosha na uwezo mkubwa wa kufanya kazi. Kuna haja ya kuwa karibu na wananchi kama tunataka kumaliza malalamiko mengi kutoka kwao", amesisitiza Naibu Waziri Aweso.

Aweso amesema Wizara ya Maji itahakikisha jambo hili linatekelezeka ili miradi yote iweze kukamilika na kuleta tija kwa wananchi na kumtaka Mhandisi wa Wilaya ya Kilolo kuomba radhi kwa wananchi kwa kosa la kitaalamu na kumtaka arekebishe changamoto hiyo.

Wilaya ya Kilolo imekamilisha utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji 10 vikiwemo Kipaduka, Ikuka na Mtono na kuongeza idadi ya wakazi wanaopata maji kufikia asilimia 71 hadi Disemba 2017 kutoka asilimia 58 mwaka 2013.

Pia, Wilaya ya Kilolo imeanza utekelezaji wa miradi mipya ya WSDP II mara baada ya kukamilisha taratibu za usanifu katika vijiji vya Lundamatwe, Kitelewasi na Ilambo ambayo imefikia asilimia 90 ya utekelezaji kwa sasa na inatarajiwa kuongeza idadi ya wakazi wanaopata huduma ya majisafi kwa zaidi ya watu 6,232.