Habari

Imewekwa: Mar, 09 2019

Naibu Waziri Aweso Ahimiza Uaminifu kwa Watendaji kwenye Utekelezaji wa Miradi ya Maji

News Images

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amewahimiza watendaji wote wa Sekta ya Maji kuwa waaminifu katika utekelezaji wa miradi ya maji ili iweze kuwa na tija.

Kauli hiyo ameitoa wakati akifunga kikao cha siku 3 kilichokutanisha wadau wa sekta hiyo jijini Dodoma kwa dhumuni la kuwapa uelewa mpana kuelekea uanzishwaji wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA).

Naibu Waziri Aweso amesema katika Sekta ya Maji kuna watumishi wazuri mno ambao wanajua majukumu yao vizuri na wenye uwezo mkubwa wa kusaidia ujenzi wa miradi inayoendelea katika maeneo mbalimbali.

Nimezunguka karibu maeneo yote nchini nikikagua miradi na kujionea mambo mazuri mliyoyafanya, ingawa nimekutana pia na mapungufu mengi yanayosababishwa na utendaji usioridhisha na mfumo uliopo.

Naomba nitie wito kwenu nyote kuwa waaminifu katika kutekeleza miradi ya maji kwa manufaa ya taifa, hatutaki tena kuona uzembe ukijitokeza katika utekelezaji wa majukumu yenu.

"Tunapoelekea kuanza kwa RUWASA tuache tamaa na kugombania vyeo maana sio dira yetu, zaidi mjidhatiti na kuwa na mikakati mizuri ya kuwapatia wananchi maji", amesema Aweso.

"Ni lazima tutimize malengo ya kufika asilimia 85 kwa maji vijijini na asilimia 95 kwa upande wa maji mijini ifikapo mwaka 2020 na tuwe na mtazamo chanya wa kufikisha asilimia 100 kwa watanzania wote", alimalizia Aweso.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Barnabas Ndunguru amesema wizara kwa upande wake itaendelea kufanikisha zoezi la kupeleka fedha kwenye miradi ili iweze kukamilika kwa wakati na kusimamia watendaji wake kwa ukaribu waweze kutimiza majukumu yao kwa weledi na uwezo katika kufikia malengo ya wizara iliyojiwekea.

Mkutano huo uliwashirikisha Makatibu Tawala wa Mikoa, Wahandisi wa Mikoa, Wahandisi wa Wilaya na Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Maji nchini.