Habari

Imewekwa: May, 02 2019

Mkandarasi Apewa Siku 7 Mradi Utoe Maji

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) amempa siku saba (7) mkandarasi kukamilisha ujenzi wa Mradi wa Maji wa Kapapa katika Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo, mkoani Mbeya.

Prof. Mbarawa ametoa maagizo hayo baada ya kukagua mradi huo ambao ujenzi wake ulianza mwaka 2014.

Waziri Mbarawa amesema hafurahishwi na mradi huo kwa kutotoa huduma ya maji kwa wananchi.

Ameainisha kuwa tatizo la mradi huo ilikuwa ni usanifu uliokuwa na kasoro katika chanzo cha maji, hivyo kusababisha maji kutofika katika miundombinu ya usambazaji.

Waziri Mbarawa amesema hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kumfukuza mkandarasi na kuwakabidhi Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya Mjini (Mbeya UWASA), ambao walitafuta mkandarasi mwingine Kampuni ya Leostarf Engineering Ltd na kufanya kazi ya ujenzi wa chanzo kipya na hivi sasa imebaki hatua ya kuunganisha mabomba 65 ya chuma katika maeno yenye makorongo kisha kuunganisha katika mtandao wa wateja.

"Kwa ujumla kazi inaenda vizuri na namuagiza mkandarasi aongeze nguvu kazi, ili kila mmoja afanye kazi katika kipande chake na baada ya siku saba (7) wakazi vijiji nane (8) waanze kupata huduma ya maji" Prof. Mbarawa amesema.

Meneja Ufundi wa Mbeya UWASA, Mhandisi Ndele Mengo amesema mradi huo utanufaisha wakazi 31,000 wa vijiji nane (8) vilivyopo katika Halmashauri ya Kyela.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) amefurahishwa kwa kukamilika kwa Mradi wa Maji wa Chunya Mjini na kusema mradi huo utaleta mageuzi makubwa kwa mji huo.

Amesema mji huo umekuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma ya maji na kukamilika kwa mradi huo kumempa faraja kubwa.

Amesema kuna hitilafu ya kiungo cha bomba kuachia, hali iliyosababisha maji kutotoka. Lakini mpaka sasa mafundi wanaendelea na ukarabati na baadhi ya maeneo yameshaanza kupata maji na baada siku chache maji yatakuwa yanatoka maeneo yote yanayohudumiwa na mradi.

Mradi wa Chunya Mjini unahudumia wakazi 15,000.