Habari

Imewekwa: Jul, 10 2018

DAWASCO Chukueni Hatua Kumaliza Tatizo la Upotevu wa Maji- Mh. Prof. Mbarawa

News Images

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mh. Prof. Makame Mbarawa ameliagiza Shirika la Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam (DAWASCO) kumaliza tatizo la upotevu wa maji, jambo ambalo limekuwa likiingizia hasara kubwa Serikali kimapato.

Mh. Prof. Mbarawa ametoa maagizo hayo katika ziara yake aliyoifanya kwa ajili ya kujionea kazi ya upanuzi wa Mitambo ya Maji ya Ruvu Juu uliopo Mlandizi na Ruvu Chini uliopo Bagamoyo, mkoani Pwani pamoja na maendeleo ya mradi wa uboreshaji wa mfumo wa usambazaji maji jijini Dar es Salaam iliyofanyika chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam (DAWASA).

Amesema kuwa pamoja na hatua kubwa zinazochukuliwa na Serikali katika kuhakikisa inamaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wake kupitia DAWASA na DAWASCO, asilimia 44 ya lita milioni 504 maji yanayozalishwa kwa siku yanapotea na kuingizia Serikali hasara ya kiasi cha Sh. bilioni 4 kwa mwezi.

‘‘Serikali inapoteza fedha nyingi kutokana na upotevu wa maji, umefika wakati wa kumaliza tatizo hilo. Hivyo nawaagiza DAWASCO kwa kushirikiana na DAWASA mhakikishe mnachukua hatua kumaliza tatizo hili mara moja. Ili maji haya yaweze kuwafikia wananchi wengi zaidi, ukiachilia mbali kuiongezea mapato Serikali,’’ aliongeza Prof. Mbarawa.

Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Dkt. Sufiani Masasi amesema kuwa mamlaka hiyo itashirikiana na DAWASCO kuhakikisha wanamaliza tatizo hilo la upotevu wa maji. Ambapo, kulingana na taarifa ya DAWASCO tatizo hilo limepungua kutoka asilimia 57 na kufikia 44 kwa sasa na jitihada kubwa zinafanyika ili kufikia lengo la kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2020.

Wakati huo, Prof. Mbarawa amemshukuru Rais, Dkt. John Magufuli kwa uteuzi wa Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali Davis Mwamunyange kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya DAWASA na kusema kuwa uteuzi huo utaleta mapinduzi katika utendaji wa mamlaka hiyo na kuongeza huduma bora ya majisafi na salama na majitaka kwa wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na maeneo ya Pwani.