Taarifa kwa Umma

TANZANIA NA BENKI YA DUNIA WASAINI DOLA MILIONI 350 ZA MAREKANI KUSAIDIA PROGRAMU YA MAENDELEO YA MAJI VIJIJINI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia (WB) wamesaini mkataba wa kiasi cha Dola za Marekani Milioni 350 (takribani Shilingi Bilioni 800) kwa ajili utekelezaji wa Programu Endelevu ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (SRWSSP) katika Wilaya 86 za Mikoa 17 ya Tanzania Bara.

Programu hii itatekelezwa kwa kipindi cha miaka 6 kuanzia mwaka 2018 hadi 2024. Utekelezaji wa programu hii utaratibiwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Lengo kuu la programu hii ni kuongeza idadi ya watu wanaopata huduma ya majisafi na salama vijijini, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa lengo la kufikia asilimia 85 ya watu wanaopata majisafi na salama vijijini ifikapo mwaka 2020.

Programu italenga maeneo makubwa manne (4):-

i. Ukarabati wa miradi ya usambazaji maji vijijini.

ii. Ujenzi wa miradi mipya ya usambazaji maji vijijini.

iii. Upanuzi wa miundombinu ya usafi wa mazingira.

iv. Kuimarisha uwezo wa taasisi katika utoaji huduma ya majisafi na usafi wa

mazingira vijijini.

Matokeo tarajiwa baada ya kukamilika kwa programu hii ni:-

i. Watu 2,500,000 kufikiwa na huduma ya majisafi.

ii. Watu 4,000,000 kufikiwa na huduma ya usafi wa mazingira.

iii. Vijiji 1,250 kufaidika na huduma ya majisafi na salama.


Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Maji na Umwagiliaji

07.09.2018