Mabonde ya Maji

Bonde la Kati

Bonde hili linajumuishwa na Mito na Vijito vinavyoingiza maji yake katika Ziwa Ambali linapatikana katika Kanda ya Kati ya Kaskazini. Vijito vidogovidogo vinavyotoka Ziwa Natron mpakani mwa Kenya kuelekea Tanzania kwenye bonde la Bahi. Eneo la bonde kwa upande wa Tanzania ni kilometa za mraba 153800. Maziwa makuu inayomwaga maji katika bonde hili ni Ziwa Eyasi linalopokea maji kutoka katika Mto Wembere na Manonga iliyopo Kaskazini mwa Tabora na Mashariki mwa Shinyanga. Ziwa Manyara hupokea maji yake kutoka kwenye ardhi chepechepe ya Bubu. Maziwa mengine madogo yaliyopo katika bonde hili ambayo hayamwagi maji yake nje ni ziwa Basuto na Natron. Bonde hili liko katika maeneo kame ya Tanzania, ambapo wastani wa mvua kwa mwaka ni kati ya 500 Milimita katika maeneo ya Bahi na 900 Milimita katika vilima vya Mbulu.

Bonde la Ziwa Tanganyika

Bonde la Ziwa Tanganyika liko Magharibi mwa nchi ya Tanzania, Bonde hili linajumuisha mabonde yote madogo yanayomwaga maji yake katika ziwa Tanganyika. Bonde lina ukubwa wa kilometa za mraba 239,000 na ukubwa wa ziwa lenyewe ni kilometa za mraba 32,000. Eneo la ardhi kwa upande wa Tanzania ni kilometa za mraba 151,000 ni sawa 60% ya maji yanayoingia ziwa Tanganyika. Sehemu kubwa ya bonde ni Mto Malagarasi yenye ukubwa wa Kilometa za mraba 130,000.

Mto Malagarasi umeanzia katika maeneo ya milima ya mpakani mwa Burundi na Tanzania katika muinuko wa 1750 kutoka usawa wa bahari. Mto unateremka Kaskazini mashariki kupitia kwenye vilima na miteremko kuelekea kwenye ardhi chepechepe ya Malagarasi. Vijito vikuu vya mto Malagarasi ambavyo ni Myowosi na Igombe vinakutana katika Ziwa Nyamagoma. Mito ya Ugala na Ruchungi inakutana na mto Malagarasi upande wa chini wa Ziwa Nyamagoma, Kwa upande wa Magharibi unapita kwenye majabali ya Misito ambapo yanatengeneza maporomoko kabla ya kuingia Ziwa Tanganyika. Mto Ugala unapokea maji kutoka katika eneo la kilometa za mraba zipatazo 52,000 na kabla haujakutana na mto Malagarasi unapita katika maeneo oevu na kutengeneza Ziwa la muda la Ugala na Sagara.

Vijito vingine vikubwa ni Ruchungi unaopokea maji kutoka vilima vya kaskazini vya Kasulu kuelekea upande wa kusini na kupitia katika maeneo oevu kabla ya kuingia mto Malagarasi maeneo ya Uvinza. Pamoja na mto Malagarasi Ziwa Tanganyika pia linapokea maji kutoka katika mabonde madogo madogo, upande wa kaskazini Magharibi wa Kigoma kuna mto Luiche, ambao hufurika wakati wa mvua.

Bonde la Wami Ruvu

Bonde le wami Ruvu linajumuisha mito mikuu miwili ambayo ni Wami wenye kilometa za mraba 400000 na Ruvu kilometa za mraba 17700. Pamoja na mito ya ukanda wa Pwani iliyopo Kusini mwa Dar es salaam. Bonde hili kwa ujumla linaukubwa km za mraba 72930 pia lina maeneo ya tambarare na safu ndefu za milima.
Kuna aina nne za milima katika bonde hili ambazo ni:

Milima ya Uluguru iliyopo Kusini Mashariki (altitude 400 mpaka 2500m

Milima ya Nguru iliyopo Magharibi ya Kilosa (altitude 400 mpaka 2000m)

Milima ya Rubeho iliyopo Magharibi ya Kilosa (altitude 500 mpaka 1000m)

Milima ya Ukaguru iliyopo Kaskazini mwa Wami (altitude 400 mpaka 1000m)

Bonde la Ziwa Victoria

Bonde la Ziwa Victoria ndani yake kuna Ziwa Victoria ambalo ni ziwa kubwa kuliko yote Barani Afrika na chanzo cha mto White Nile. Ziwa Victoria lipo katika Latitudi 031 Kaskazini na 354 Kusini, na Longitudi 3118 Mashariki na 3454 Magharibi. Lina wastani wa kina cha mita 80. Ziwa hili linajumuisha nchi 3 ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda. Mito ambayo inamwaga maji Ziwa Victoria ni pamoja na Mto Kagera, Simiyu, Mbarageti, Gurumeti, Mara na Mori. Upande wa Mashariki wa bonde hasa katika miinuko ya Tarime, misimu ya mvua ni miwili, wakati upande wa Kusini wa bonde ambao ni mkoa wa Mwanza kuna msimu wa mvua na kiangazi, na upande wa Magharibi unapata mvua kipindi chote cha mwaka na mvua chache katika mwezi wa saba. Kiasi cha wastani wa mvua kwa mwaka kinatofautiana katika maeneo mbalimbali ya ziwa na maeneo yanayolizunguka. Upande wa Mashariki wastani wa mvua kwa mwaka ni kati ya 500 na 700mm. Upande wa Magharibi mvua huongezeka hadi kufikia wastani 2000mm katika maeneo ya Bukoba na visiwa vya Ssese. Upande wa kusini mwa ziwa katika maeneo ya Mwanza wastani wa mvua ni kati ya 750-1100mm na upande wa Mashariki katika maeneo ya Mara wastani wa mvua kwa mwaka ni kati ya 750-1000mm na huongezeka hadi 1600mm katika miinuko ya Tarime.

Bonde la Mto Ruvuma

Bonde la Mto Ruvuma na Pwani ya Kusini lina mito mikuu mitano inayomwaga maji yake katika bahari ya Hindi. Mito hiyo ni Mto Matandu wenye kilometa za mraba 18,565, Mto Mavuji wenye kilometa za mraba 5,600, Mto Mbwemkuru wenye kilometa za mraba 16,255, Mto Lukuledi wenye kilometa za mraba 12950 na vijito vya mto Ruvuma Maeneo ya mabonde madogo yapo kati ya altitudi 305-710 juu ya usawa wa bahari, na hutiririsha maji yake kuelekea ukanda wa pwani. Mto Ruvuma unashirikiana kati ya Tanzania na Msumbiji na unamwaga maji yake katika bahari ya Hindi. Mto huu una urefu wa kilometa 800 kati ya hizo kilometa 650 zipo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji. Bonde la mto Ruvuma lina ukubwa wa kilometa za mraba 152,200 kati ya hizo kilometa 52,200 (34.3%) zipo Tanzania na kilometa 99,530 (65.39%) zipo Msumbiji na Malawi kilometa 470 (0.31%). Vijito vikubwa vya mto huu kwa upande wa Tanzania vimeanzia katika wilaya za Mbinga, Tunduru na Masasi. Wastani wa maji yanayoingia mto Ruvuma kwa mwaka ni mita za ujazo 15,000 milioni. la mto Ruvuma na pwani ya kusini lina ukubwa wa kilomita za mraba 104,270 na idadi ya watu wapatao 2,241,944. Wastani wa nyuzi joto ni 260C kwa ukanda wa pwani na nchi kavu nyuzi joto 24, mabadiliko ya hali ya joto kwa siku na mwaka hutokea

Bonde la Mto Rufiji

Ofisi ya Maji Bonde la Rufiji inayosimamia matumizi ya maji katika Bonde la Rufiji. Bonde hili maana yake ni eneo lote ambalo mwelekeo wa maji yake huingia Mto Rufiji na hatimaye Bahari ya Hindi. Bonde hilo lina eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 177,420 na lina mito mikuu minne ambayo ni Great Ruaha Mkuu wenye eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 82,970, Kilombero wenye eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 39,990. Mto mwingine ni Luwegu wenye eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 26,300 na Mto Rufiji wenye eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 22,160. Ofisi ya Bonde la Rufiji iko katika Mkoa wa Iringa barabara ya Dodoma. Kimuundo ofisi hiyo iko chini ya Idara ya Rasilimali za Maji katika Wizara ya Maji. Hutekeleza malengo yake kwa kushirikiana na ofisi za Halmashauri za Wilaya zote zilizoko kwenye Bonde hilo. Bonde hilo lina Bodi yake ambayo ina wajumbe kumi ambapo Afisa Maji wa Bonde ndiye Katibu wa Bodi hiyo. Bodi na ofisi ya Bonde la Rufiji ilianzishwa Septemba 1993, kwa mujibu wa Sheria ya Maji Na.42 ya mwaka 1974 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 1981 na 1991. Aidha, Waziri mwenye dhamana ya rasilimali za maji ndiye mteuzi wa Bodi hiyo.