Habari

Imewekwa: Jan, 31 2019

Waziri wa Maji Mhe. Prof. Makame Mbarawa asoma Muswada wa Sheria ya Maji na Usafi wa Mazingira Bungeni

News Images

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) leo amesoma Muswada wa Sheria ya Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira wa Mwaka 2018 (The Water Supply and Sanitation Bill of 2018) pamoja na marekebisho yake.

Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) akiwasilisha hoja Bungeni, amewaomba Waheshimiwa Wabunge wajadili Muswada huo wenye lengo la kuboresha huduma ya maji nchini. Amesema Muswada huo umelenga kutungwa kwa sheria mpya ya huduma ya maji na usafi wa mazingira ambayo itaweka utaratibu wa kisheria katika kusimamia utoaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira nchini.

Pia sheria hiyo inalenga kufutwa kwa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Namba 272 na Sheria ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASA) Sura 273 ili kuwa na sheria moja itakayosimamia shughuli zote za utoaji huduma ya majisafi na usafi wa mazingira katika ngazi mbalimbali nchini.

Mambo muhimu yaliyozingatiwa katika Muswada ni kama yafuatayo:-

- Kubainisha majukumu ya watendaji katika ngazi mbali mbali,

- Kuendelea kutambuliwa kwa mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira nchini,

- Kuendelea kutambua na kuanisha majukumu ya EWURA,

- Kuanisha ushiriki wa jamii kwa kuanzishwa vyombo vya watumia maji,

- Kuanzishwa kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASSA),

- Kuendelea kutambuliwa kwa uanzishwaji wa Mfuko wa Taifa wa Maji (NWIF)

- Kuwekwa makosa na adhabu chini ya sheria hii, masharti ya ujumla na masharti ya mpito.

Matokeo tarajiwa chini ya sheria hii ni pamoja na:-

- Kuongezeka kwa ufanisi na uwajibikaji,

- Kuimarika kwa ujenzi, usimamizi na uendeshaji wa miradi ya maji,

- Uendelevu wa miradi ya maji vijijini,

- Uendelevu wa huduma za maji nchini na kuchochea utendaji katika sekta nyingine,

- Kuwa sheria moja katika kusimamia sekta ya usambazaji maji nchini.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano

31 Januari, 2019