Habari

Imewekwa: May, 25 2019

Waziri wa Maji Ahimiza Usimamizi Mzuri wa Miradi ya Maji

News Images

TAARIFA KWA UMMA

Waziri wa Maji Mhe, Profesa Makame Mbarawa (Mb) amesisitiza umuhimu wa Wataalam wa Sekta ya Maji kusimamia miradi ya maji kwa ufanisi ili kuweza kuwa na miradi yenye tija inayolingana na thamani ya fedha zinazowekezwa na Serikali kwenye miradi yote nchini.

Profesa Mbarawa amesema ni lazima kuwe na usimamizi mzuri kwa kila hatua ya utekelezaji wa miradi ya maji, ili kuweza kupata matokeo yanayotarajiwa baada ya kukamilika kwa miradi hiyo, ambayo ni kumaliza tatizo la maji nchini kote.

Akitoa majibu kwa mkandarasi aliyekuwa akilalamika kucheleweshewa malipo na Serikali, Profesa Mbarawa amesema jambo hilo linatokana na tabia ya wakandarasi kuweka makisio makubwa ya gharama za miradi ya maji kwa dhumuni la kupata faida kubwa, kulinganisha na gharama halisi za ujenzi wa miradi hiyo. Wakandarasi wengi wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya wahandisi wasio waaminifu kuihujumu Serikali na kusababisha kushindwa kulipa fedha hizo kwa wakati kutokana na gharama kuwa kubwa kupita kiasi.

“Tumegundua tulikuwa tukiibiwa fedha nyingi, hivi sasa tumeweka utaratibu wa kujiridhisha na makisio ya gharama za kila mradi kwa kila kipengele, kabla ya kuingia mkataba. Hatua hii imetusaidia kupunguza gharama kwa kulipa gharama zinazostahili. Hivyo, kutuwezesha kulipa wakandarasi kwa wakati na kuwa na miradi yenye viwango bora inayokamilika kwa wakati’’, Profesa Mbarawa amesema.

Profesa Mbarawa ameanza ziara ya kikazi mkoani Katavi leo kwa kutembelea miradi ya maji ya Manga, Ikolongo II, Igagala, Ngomalusambo na Kabungu akiridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya maji kwa ujumla mkoani humo.


Kitengo cha Mawasiliano

Mei 25, 2019