Habari

Imewekwa: Sep, 21 2018

Wakazi wa Ikozi Kupata Maji Ndani ya Miezi Sita

News Images

Wakazi wa Kijiji cha Ikozi, Wilaya ya Sumbawanga Vijijini, mkoani Rukwa wanatarajia kupata huduma ya majisafi na salama mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Bwawa la Maji utakaoanza kutekelezwa hivi karibuni.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa mara baada ya makabidhiano ya mkataba wa ujenzi wa bwawa hilo na Mkandarasi wa Kampuni ya Emirate Builders na linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita ijayo.

Akizungumza katika makabidhiano hayo mbele ya wakazi wa kijiji hicho, Profesa Mbarawa amemwagiza mkandarasi huyo kumaliza kazi hiyo ndani ya miezi sita kulingana na mkataba, vinginevyo atamchukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kumfutia usajili kwenye Bodi ya Wakandarasi nchini.

Akimwambia kuwa ni wajibu wake kuifanya kazi hiyo kwa haraka na kwa kiwango bora ili kutimiza lengo la Serikali la kuwapatia wananchi maji, huku akisisitiza ni lazima tatizo la maji liishe Rukwa na nchi nzima kwa kuwa fedha za kutekeleza miradi ipo.

‘‘Mkandarasi huyu amekuwa akifanya vizuri kwenye miradi yetu mingi ya maji, ninategemea ataifanya kazi hii vizuri na italingana na thamani halisi ya fedha takribani Sh. Bilioni 2 tuliyowekeza kwenye mradi huu. Pia, akawataka wakazi wa kijiji hicho kutunza na kulinda miradi ya maji ambayo Serikali imewekeza kiasi kikubwa cha fedha’’, alisema Profesa Mbarawa.

Wakati huo, Profesa Mbarawa ameiagiza Mamlaka ya Maji mjini Sumbawanga kuhakikisha inaongeza mtandao wa maji katika maeneo ya makazi mapya kwa kuwa mradi mkubwa uliokamilika wa Sumbawanga mjini unatosha kutoa huduma ya uhakika katika wakazi wa mji huo.

Akiwa katika ziara yake ya kukagua mradi huo, Profesa Mbarawa ameridhishwa na ujenzi wa mradi huo na kusema kuwa Serikali imewekeza zaidi ya Sh. Bilioni 30 kwa ajili ya kumaliza tatizo la maji mjini Sumbawanga na maeneo ya jirani.

Mkoa wa Sumbawanga unakadiriwa kuwa na jumla ya wakazi 1,004,539 na mpaka kufikia Juni, 2018 asilimia 52 wanapata huduma ya maji kupitia miradi 235 ya mkoa huo iliyojengwa chini ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) na programu nyingine za NORAD, RUDEP, TASAF na Quickwins ambayo imesaidia kupunguza changamoto za upatikanaji wa maji kwa wananchi.