Habari

Imewekwa: May, 24 2019

Vijiji 10 Sumbawanga Kunufaika na Mradi Mkubwa wa Maji wa Muze Group

News Images

TAARIFA KWA UMMA

Vijiji 10 vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa vinategemea kunufaika na huduma ya majisafi na salama kupitia Mradi mkubwa wa Maji wa Muze Group unaotegemewa kuanza utekelezaji wake mwezi Juni mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa alipotembelea maeneo ya vijiji mradi huo utakapopita na chanzo cha maji cha mradi huo cha Mto Kilambwa kwa dhumuni la kujiridhisha na mpango kazi wa utekelezaji wa mradi huo utakaochukua miezi 12 kukamilika.

Profesa Mbarawa amesema hatua ya usanifu ya mradi huo imeshakamilika na utagharimu Shilingi bilioni 6.2, ingawa anaangalia kama upo uwezekano wa kupunguza gharama hizo kufikia Shilingi bilioni 3.5 ili kuokoa fedha zitakazobaki na kuweza kufanya kazi nyingine.

‘‘Nimekuja kujiridhisha baada ya kupokea taarifa ya usanifu ya mradi pamoja na gharama zake za utekelezaji mpaka unakamilika. Kulikuwa na umuhimu wa kuja kuona mpango mzima wa ujenzi wa mradi huu na kupata picha halisi kabla ya kuidhinisha fedha na kuanza kazi rasmi’’, Profesa Mbarawa amezungumza.

Akiwa kwenye sehemu ya muendelezo wa ziara yake katika Mkoa wa Rukwa, Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amewataka wananchi wawe wavumilivu kwani mara baada ya kukamilika kwa mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni tatu na nusu kwa siku, utasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua kero ya upatikanaji wa maji iliyodumu kwa miaka mingi wilayani humo.

‘‘Nimeridhika na chanzo cha maji cha Mto Kilambwe kina maji ya kutosha kwa ajili ya mradi huu unaotarajiwa kuanza mwezi ujao na utakamilika baada ya miezi 12’’, Profesa Mbarawa amesema.

Wakati huohuo, Diwani wa Kata ya Muze, Kalolo Ntilla amesema ujio wa Waziri wa Maji utaleta matumaini makubwa kwa wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa na kilio cha huduma ya majisafi na salama kiasi cha kuona kama wamesahaulika na Serikali yao. Huku akitoa ahadi wananchi wako tayari kushiriki kwa asilimia 100 katika kufanikisha ujenzi wa mradi huo wa kihistoria.


Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Mei 24, 2019