Habari

Imewekwa: May, 22 2019

Serikali Kutumia Bilioni 2.9 Kumaliza Tatizo la Maji Sumbawanga

News Images

TAARIFA KWA UMMA

Serikali imepanga kutumia zaidi ya Shilingi bilioni 2.9 kwa ajili ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Ikozi ikiwa ni miongoni mwa Miradi ya Maji 6 inayotekelezwa chini ya Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Maji awamu ya Pili (WSDP II) katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa yenye lengo la kutatua kero ya upatikanjai wa maji kwa wananchi.

Akizungumza na wananchi wa Ikonzi mara baada ya kutembelea baadhi ya miradi ya Wilaya ya Sumbawanga, Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali imejipanga kutekeleza na kusimamia mradi huo kwa ufanisi na kuwa mradi wa ujenzi wa bwawa wa mfano kwa kuzingatia viwango vya ubora na usalama kwa wananchi walio karibu na mradi huo.

Profesa Mbarawa amesema miradi mingi ya mabwawa nchini imekuwa ikitekelezwa chini ya viwango na ikishindwa kutimiza lengo halisi, akisisitiza wizara itasimamia kwa ukaribu utaratibu mzima na maendeleo ya ujenzi wa bwawa hilo ili liweze kuwa mfano wa kuigwa nchini.

‘‘Mradi huu ulianza Novemba, 2018 chini ya mkandarasi wa Kampuni ya Emirate Builders Ltd kwa gharama ya Shilingi bilioni 2,943,086,780 na ameshalipwa asilimia 15 ya malipo ya awali Shilingi 441,463,017 unatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2019’’, Profesa Mbarawa ameeleza.

‘‘Mkataba wa mradi huu unahusisha ujenzi wa bwawa la ujazo wa lita 436,015,120 pamoja na kazi nyingine na awamu ya kwanza unatarajia kuhudumia Vijiji (3) vya Ikozi, Kazwila na Chituo vyenye jumla ya wakazi 14,395 na baada ya hapo huduma itasogezwa mpaka Kijiji cha Tentula chenye idadi ya wakazi 2,452’’, Profesa Mbarawa amesema.

Mhandisi wa Maji Wilaya ya Sumbawanga, Patrick Ndimbo amesema usimamizi wa kazi ni mzuri, mkandarasi amekuwa akitumia muda mwingi akiwa site na kazi hiyo inaendelea vizuri akitegemea kukabidhiwa kazi hiyo ifikapo mwezi Julai kama mkataba unavyoonyesha.

Awali, Profesa Mbarawa alitembelea Mradi wa Maji wa mji mdogo wa Laela na kutoridhishwa na mkandarasi anayetekeleza awamu ya pili ya mradi huo na kuagiza akutane mkandarasi huyo, ili wapange pamoja upya mpango kazi wa utekelezaji wa mradi huo uliotegemewa kukamilika baada ya miezi minne jambo ambalo waziri huyo amelikataa.

Akiwa katika mradi huo ameagiza chanzo kipya cha mserereko (gravity) cha Kimenyanze kitumike baadala ya chanzo cha awali, kwa kuwa nguvu ya umeme wa nishati ya jua (solar) zilizokuwa zimefungwa kushindwa kusukuma maji kutoka kwenye chanzo hicho cha awali kwenda kwenye tenki na kuyasambaza kwa wananchi.

Profesa Mbarawa amesema jumla ya gharama za mradi huo ni zaidi ya Shilingi bilioni 1.7 na zaidi Shilingi bilioni 1.4 sawa na asilimia 80 zimeshalipwa, akatoa miezi miwili tu kwa mkandarasi mradi huo uwe umekamilika.

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Mei 22, 2019