Habari

Imewekwa: Sep, 21 2018

Profesa Mbarawa Aziagiza Halmashauri Kutowapa Kazi Wakandarasi Wasio na Uwezo

News Images

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amezitaka halmashauri zote nchini kutowapa miradi wakandarasi wasio na uwezo kwa kuwa ndio chanzo kikubwa cha matatizo ya miradi mingi ya maji.

Profesa Mbarawa ametoa agizo hilo mara baada ya kupewa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji Kirando, wilayani Nkasi katika mkoa wa Rukwa ambao utekelezaji wake umekwama kwa muda mrefu kutokana na uwezo mdogo wa mkandarasi.

Profesa Mbarawa amepiga marufuku mkandarasi ambaye hana rekodi nzuri ya kukamilisha kazi alizopewa kupewa mradi zaidi ya mmoja, baada ya kubaini wakandarasi wengi wamekuwa wakipewa kazi tofauti kwenye maeneo mbalimbali wakati kazi zao ni za kusuasua katika kila miradi wanayoitekeleza.

Huku akizitaka halmashauri hizo kuthibitisha uwezo wa mkandarasi na kazi alizokwishafanya ili kuepusha hasara kwa Serikali ambayo imekuwa ikitoa fedha nyingi za miradi bila faida.

‘‘Tumeanza kujenga miradi yenye thamani halisi ya fedha tunazowekeza kwenye miradi ya maji, hatutakubali tena wakandarasi wasio na uwezo waendelee kula fedha za walipa kodi. Ni lazima kuanzia sasa tujidhirishe na kila mkandarasi kwa lengo la kuokoa fedha za walipa kodi kwa kuwa na miradi bora na endelevu’’, alisema Profesa Mbarawa.

Wakati huo Profesa Mbarawa amesema atatuma mara moja timu ya wataalamu kutoka wizarani ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Sumbawanga mjini (SUWASA), Mhandisi Hamisi Makalla kufanya upya ya upembuzi yakinifu wa mradi wa Kirando kabla ya kumtafuta mkandarasi atakayeanza kazi hiyo kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda amesema atahakikisha mkandarasi atakayepewa kazi hiyo anakuwa na uwezo wa kufanya kazi hiyo kwa kiwango na kusisitiza yuko tayari kufanya kazi ya usimamizi usiku na mchana ili ikamilike kwa wakati.

Mradi huo wa maji awali ulikumbana na changamoto za ubadhirifu wa fedha, hali iliyosababisha Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuagiza kufanyika uchunguzi na kukamatwa kwa watuhumiwa kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.