Habari

Imewekwa: May, 28 2019

Profesa Mbarawa Amchukulia Hatua Mkandarasi Makambako

News Images

TAARIFA KWA UMMA

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) ametoa onyo kali kwa wakandarasi wa miradi ya maji kuhakikisha wanaacha tabia ya ubabaishaji na kufanya kazi zao kwa kuzingatia weledi na kuheshimu mikataba wanayoingia na Serikali wakati akikagua Mradi wa Maji wa Bwawani, mjini Makambako, mkoani Njombe.

Kauli hiyo ameitoa mara baada kukuta ujenzi wa mradi huo unaotegemewa kuongeza huduma ya maji kwa wakazi 4,837 sawa na asilimia 67 Makambo mjini, imesimama kwa muda mrefu na mkandarasi kutokuwepo “site” huku wakazi wa mji huo wakiendelea kuwa na tatizo la huduma ya maji.

.

Hali iliyosababisha Waziri wa Maji kumtaka Mkandarasi kutoka BWE Co. Ltd kutoa maelezo kuhusu kusimama kwa kazi hiyo na yeye kutoonekana eneo la kazi, ambapo sababu zake zikionekana kukinzana na makubaliano ya mkataba wa utekelezaji wa mradi huo. Hivyo kumlazimu Profesa Mbarawa kuelekeza vyombo vya usalama kumkamata na kumtaka ahakikishe anajipanga kumaliza kazi ya ujenzi wa mradi haraka iwezekanavyo, vinginevyo atamchukulia hatua kali zaidi ikiwemo kumfutia usajili kwenye Bodi ya Wakandarasi nchini.

Aidha, Profesa Mbarawa ametembelea Mradi wa Maji wa Mbalizi na kukagua ujenzi wa chanzo kilichopo Mto Mbalizi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, mkoani Mbeya kwa dhumuni la kusukuma kasi utekelezaji wa mradi huo uweze kukamilika kwa wakati. Ujenzi wa mradi huo utachukua miezi sita (6) na unatarajiwa kutoa huduma kwa wakazi wapatao 150,000 wanaoishi kwenye mji mdogo wa Mbalizi, mkoani Mbeya.

Hatua hiyo ya ufuatiliaji wa miradi ya Maji ya Bwawani na Mbalizi inatokana na agizo la Mhe. Rais John Magufuli la kutaka tatizo la maji kwa wananchi wa maeneo hayo litatuliwe mara moja, baada ya kusikia kero zao wakati wa ziara yake ya kikazi katika mikoa ya Njombe na Mbeya hivi karibuni.

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Mei 27, 2019