Wasifu

Mhe.  Isack Kamwelwe (Mb)

Waziri wa Maji na Umwagiliaji

Mhe. Isack Kamwelwe (Mb)

Akiwa amezaliwa tarehe 30 Aprili 1956 mkoani Katavi, Mheshimiwa Mhandisi Isack Aloyce Kamwelwe ana Shahada ya Uzamili (2007-2009) na Stashahada ya Juu (2005-2006) katika Menejimenti ya Uhandisi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Aidha, Mhandisi Kamwelwe alihudhuria mafunzo na kutunukiwa Astashahada ya Ufundi (FTC) mwaka 1980-1984 na Stashahada ya Ufundi mwaka 1988-1991 katika kilichokuwa Chuo cha Ufundi, Dar es Salaam. Mhandisi Kamwelwe alisoma elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Ilunde, Katavi (1968-1975) na elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari ya Ufundi, Moshi (1976-1979).

Kabla ya kuingia katika siasa kama Mbunge wa Katavi mwaka 2015, Mheshimiwa Mhandisi Kamwelwe alifanya kazi kama Fundi (1984-1992) na Mhandisi Mkuu (1993-2007) katika Wizara ya Ujenzi. Mhandisi Kamwelwe alipanda ngazi na kuwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), nafasi ambayo aliitumikia kati ya 2007 na 2011, kabla ya kuteuliwa kuwa Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Katavi mwaka 2011, nafasi ambayo aliitumikia hadi alipostaafu mwaka 2015.

Mheshimiwa Mhandisi Isack Aloyce Kamwelwe alitajwa kuwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji katika Baraza la Mawaziri la kwanza la Rais John Pombe Magufuli alilolitangaza mwezi Novemba 2015. Mheshimiwa Mhandisi Kamwelwe aliteuliwa kwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji mwezi Oktoba 2017 kufuatia mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Magufuli.