| Ujumbe kutoka kwa Waziri |  |
Karibu katika Tovuti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji
Maji ni hitaji muhimu na haki ya kila kiumbe hai. Yatunze na yathamini, kuwepo kwetu na maendeleo yetu tunayategemea. Wajibu wa Wizara hii ni kuendeleza na kusimamia rasilimali za maji hapa nchini. Madhumuni ya Tovuti ni kuweka jukwaa la mawasiliano kati ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji, wadau wake na umma kwa ujumla. Vilevile itasaidia upatikanaji wa habari za kila siku za Wizara ambazo ni muhimu kwa umma.
Maji ni muhimu kwa maisha na mazingira, ni muhimu katika shughuli za kiuchumi na kijamii, yanagusa nyanja zote za maisha ya binadamu, hii ni pamoja na: matumizi ya nyumbani, mifugo, uvuvi, wanyamapori, viwanda, nishati, burudani na shughuli zingine za kijamii na kiuchumi. Maji ni nguzo muhimu katika kupunguza umaskini kama vile usalama wa chakula, usafi wa mazingira na majumbani. Upatikanaji wa majisafi na salama hukuza kiwango cha maisha, ilhali ukosefu wa majisafi na salama husababisha kushuka kwa kiwango cha maisha bora pamoja na umri wa kuishi.
Vyanzo vikuu vya maji baridi hapa nchini ni: Maziwa, mito, chemchemi, mabwawa na maji chini ya ardhi.
Hata hivyo, maji haya hayapo katika uwiano ulio sawa, baadhi ya maeneo ya nchi yetu hayana uwiano ulio sawa wa vyanzo vya maji, mengine hupata maji musimu wa mvua tu, mengine yanapata maji mwaka wote na mengine hayana chanzo chochote.
Ongezeko la idadi ya watu mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kukua kwa miji kumeathiri upatikanaji wa maji yaliyopo. Kuwepo kwa maisha endelevu ya wanadamu na mazingira kunategemea kuwepo kwa mipango mizuri ya usimamizi na uendelezaji wa vyanzo vya maji.
Sera ya Maji ya mwaka 2002 imeweka mwongozo mzuri wa maendeleo endelevu ya Sekta ya maji hii ni pamoja na kuendeleza, kusimamia pamoja na matumizi endelevu ya vyanzo vya maji.
Ili kutekeleza Sera ya Maji, Wizara imeandaa Mkakati wa Maendeleo wa Sekta ya Maji nchini 2006-2015 pamoja na Programu ya Maendeleo ya Maji ya mwaka 2006-2025. Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Maji nchini unafafanua kazi na majukumu ya wadau na vipaumbele katika utekelezaji wa Sera ya Maji.
Kumbuka kwamba mabadiliko ya kweli yanajenga msingi madhubuti kwa mahitaji ya baadaye.
“Maji ni uhai na usafi wa mazingira ni utu.”
Ahsante
|