Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tanzania yashiriki Mkutano wa Mazingira wa Nchi za Mashariki ya Kati na Afrika

Swahili

Tanzania imeshiriki Mkutano wa Kimataifa wa Mashariki ya Kati na Afrika wa Mazingira “Middle East-Africa Environment Forum” uliofanyika Juni, 8-9 katika Jiji la Seoul, nchini Korea.  Mkutano huo wa kimataifa uliandaliwa na Serikali ya Korea ulilenga kubadilishana maaarifa na uzoefu katika masuala ya utunzaji mazingira na utoaji wa huduma bora ya maji na usafi wa mazingira, pamoja na kuendeleza ushirikiano katika masuala ya uwekezaji baina ya nchi za Afrika, Mashariki ya Kati na Korea.  Katika Mkutano huo, ambapo Tanzania iliwakilishwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji chini ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Inj. Emmanuel Kalobelo, ambaye alipata nafasi ya kukutana na kunadi fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania katika miradi ya maji na umwagiliaji, mbele ya Makamu Waziri wa Mazingira wa Korea, Dkt. Jeong Yeon-man na kubadilishana uzoefu kuhusiana na masuala ya mazingira.

Pia, alifanikiwa kukutana na wawekezaji wa Korea, Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na wawakilishi wa nchi mbalimbali kutoka Afrika na Mashariki ya Kati zikiwemo Zambia, Kenya, Iran, Burkina Faso, Misri na Msumbiji. Inj. Kalobelo alipata nafasi ya kuonyesha fursa zilizopo nchini Tanzania wakati akiwasilisha mada yake katika mkutano huo, na kuzivutia Serikali ya Korea pamoja na Sekta zake Binafsi kwa fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta za Maji na Umwagiliaji, na kukubali kuongeza uwekezaji katika sekta hizo nchini na kuahidi kuzidisha ushirikiano uliopo kati yao na Tanzania. Pamoja na kutoa fursa za mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu kwa wataalamu wa Sekta Mazingira na Maji Tanzania.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu alifanya ziara kwenye makampuni mbalimbali ya Korea ambayo yameonesha nia ya kuwekeza Tanzania, kwa lengo la kubaini uwezo wa makampuni hayo katika kutekeleza miradi mikubwa ya maji na umwagiliaji ili kupata uhakika wa uwezo wa makampuni hayo katika uwekezaji huo.

Photo: