Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taarifa kwa Umma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, amezindua miradi ya upanuzi ya mtambo wa maji wa Ruvu Juu na ulazaji wa mabomba makuu katika kiwanja cha Ruvu Juu Mlandizi Mkoani Pwani. Mradi huu umetekelezwa kwa Serikali ya Tanzania na Serikali ya India kupitia Benki ya Exim kwa gharama ya shilingi bilioni 217.

Mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Juu umeongeza uwezo wa mtambo wa kusafisha na kusukuma maji na hivyo kuongeza uzalishaji maji kutoka lita milioni 82 za awali hadi lita milioni 196 kwa siku kwa sasa baada ya kukamilika, hivyo mradi huu kwa sasa umekabiliana na kasi ya ukuaji wa miji ya Mlandizi, Kibaha na Jiji la Dar es Salaam.

Kazi zilizotekelezwa katika mradi huu ni ukarabati wa kituo cha zamani cha kutoa maji mtoni, ujenzi wa kituo kipya cha kusukuma maji ghafi chenye pampu mpya 3 na kila moja inauwezo wa kusukuma maji lita milioni 68 kwa siku, ujenzi wa bomba jipya la kusafirisha majighafi lenye kipenyo cha mita 1.2 na urefu wa KM 6 kutoka Ruvu darajani hadi Mlandizi kwenye mtambo wa kusafisha maji, ujenzi wa mfumo mzima wa kusafisha na kuweka dawa maji, ujenzi wa tanki la kuhifadhia majisafi lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 10, ujenzi wa nyumba 17 za wafanyakazi, ujenzi wa njia ya umeme na ufungaji wa transfoma.

Mradi umejengwa na kampuni ya VA TECH WABAG kutoka India na umegharimu Dola za Marekani milioni 39.7 sawa na shilingi bilioni 87. Kukamilika kwa miradi hii tayari kumeanza kuimarisha huduma ya maji katka maeneo ya Mlandizi, Kibaha, na vitongoji vyake, Kibamba, Mbezi, Kimara, Kinyerezi, Segerea, na Tabata. Maeneo haya yalikuwa na uhaba mkubwa wa maji.

Ili kuhakikisha ongezeko la maji baada ya upanuzi wa mtambo yanafikia walaji, mradi huo ulijengwa sambamba na mradi wa ulazaji mabomba makuu yenye kipenyo cha mita 1.2 na urefu wa KM 40 kutoka Mlandizi hadi Kibamba, ujenzi wa bomba lenye kipenyo cha MM 900 urefu wa KM 20 kutoka Kibaha Tanita hadi Kibamba, ujenzi wa tanki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 10 eneo la Kibamba, ujenzi wa bomba lenye kipenyo cha mita 1.0 na urefu wa KM 10 kutoka Kibamba kwenye tanki jipya hadi Kimara, pamoja na ujenzi wa ofisi eneo la Kibaha kwa gharama za dola za Marekani 59.3 sawa na shilingi bilioni 130 na ilisimamiwa na kampuni ya WAPCOS LTD ya India.