Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Serikali yaridhishwa na Maendeleo ya Mradi wa Maji Chalinze

Swahili

Serikali imesema kuwa inaridhishwa na hali ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa Mtambo wa Maji Chalinze, unaohusisha ujenzi wa mfumo wa kusafirishia na kusambaza maji pamoja na matenki ya kuhifadhi maji utakaozalisha zaidi lita milioni tisa utakapokamilika. Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua mradi huo utakaonufaisha wakazi zaidi ya laki tatu wa Wilaya za Chalinze, Pwani na Handeni, Tanga, Naibu Waziri wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Inj. Isack Kamwelwe amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuona wananchi wa Chalinze wanapata huduma ya maji kwa wakati kupitia mradi huo, unaotarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu.

“Mradi wa Lindi umekamilika na hapa lazima tuchukue hatua kama Lindi, ili kutatua changamoto zinazokwamisha kukamilika kwa mradi kwa wakati  na kwa kuwa wametupa mpango kazi wao tunaamini kazi itakamilika kwa wakati na nitafuatilia kila hatua’’, alisisitiza Inj. Kamwelwe. Akifafanua Inj. Kamwele amesema kuwa ameridhishwa na kasi ya utendaji na kuipongeza Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) kwa usimamizi mzuri katika utekelezaji wa miradi ya maji wanayokabidhiwa.  Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Chalinze (CHALIWASA), Inj. Christer Mchomba amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kukuza shughuli za kiuchumi zikiwemo Sekta za Kilimo, Mifugo na Viwanda na tayari wamepokea maombi ya Viwanda vya Juisi, Kutibu Mbao, na Vigae ya kuunganishiwa huduma ya maji.

Aliongeza kuwa awamu ya tatu ya mradi huo itagharimu Sh. bilioni 84 hadi kukamilika kwake, na hatua iliyofikia sasa ni ulazaji wa mabomba ya kusafirishia maji iliyofikia umbali wa km 96.8 kati ya km 115 na ujenzi wa ofisi umefikia asilimia 82. Kwa upande wake Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji cha Rupungwi, Chalinze ambacho ni sehemu ya vijiji vinavyonufaika na mradi huo, amesema wananchi wanaipongeza Serikali kwa kuwaletea mradi huo utakaoinua shughuli za kiuchumin katika wilaya yao. Mradi huu unatekelezwa kupitia mkopo kutoka India na mkataba wa ujenzi ulisainiwa Mei 18, 2015 kati ya DAWASA na Kampuni ya Overseas Infrastracture Pvt Ltd ikishirikiana na PIL zote za India.

Photo: