Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Prof. Mkumbo aridhishwa na maendeleo wa Mradi wa Ng’apa

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo ameridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa maji wa Ng’apa uliopo mkoani Lindi, mara baada ya ziara aliyoifanya mjini Lindi. Prof. Mkumbo amefanya ziara hiyo kwa nia ya kujua hali ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa, ambao unatekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya mji wa Lindi (LUWASA), kama sehemu ya kufuatilia maagizo yaliyotolewa na Mhe. Rais John Magufuli miezi michache iliyopita wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani humo.

“Hali ya huduma ya maji Lindi si nzuri, ukizingatia inakidhi asilimia 40 tu ya mahitaji. Kwa mradi huu wa Ng’apa ukikamilika utatoa huduma ya maji kwa asilimia 100 kwa wakazi wa mji wa Lindi, ikumbukwe Mhe. Rais alifanya ziara Lindi na akatoa maelekezo kuhusu mradi huu”, alisema Prof. Mkumbo.

Prof. Mkumbo alisema kuwa ziara hiyo ni sehemu ya kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais na amefurahishwa na maendeleo ya mradi huo, na kuwa maji yameshafika na kilichobaki ni kupelekwa kwenye chujio ambalo lipo kwenye matengenezo kabla ya kuanza kusambazwa kwa wananchi. Huku akisisitiza kuwa ni wajibu wa Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi na LUWASA haina budi kutekeleza mradi huo kwa wakati kwa niaba ya Serikali.

Wakati huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (LUWASA), Inj. Riziki Chambuso alisema mradi huo umefikia hatua nzuri na watatekeleza agizo la Rais kuwa ifikapo mwezi Julai mradi utakuwa umekamilika na kuwapatia wakazi wa Lindi mjini maji. Mradi wa Ng’apa ni moja ya miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano kama sehemu ya ahadi yake na unategemea kugharimu Sh. bilioni 29, kufikia sasa Sh. bilioni 22 zimeshatolewa. Ujenzi wa mradi huo, pia utahusisha upanuzi wa miundombinu ya maji kwa maeneo ambayo hayajafikiwa na miundombinu hiyo kwa ajili ya kusambazia maji.