Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

‘Ole Wenu Wezi wa Maji’-Naibu Waziri Aweso

Swahili

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso ametoa onyo kali kwa wezi wa maji na wahujumu wa miundombinu ya maji na kuwataka waache tabia hiyo mara moja kwa kuwa Serikali imechoka kuingia gharama kubwa za utekelezaji wa miradi ya maji na kuhujumiwa. Hayo yamesemwa wakati alipotembelea Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) wakati akizungumza na Bodi, menejimenti na watumishi wa mamlaka hiyo inayotoa huduma ya maji kwa wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.

Aweso amesema wizara itaanzisha kampeni kabambe nchi nzima ya kubaini mtandao mzima na wale wote wanaoihujumu Serikali kwa wizi wa maji na miundombinu yake na kuziagiza mamlaka zote nchini kuweka mikakati mizuri ya kudhibiti tabia hiyo. Amesema miradi ya maji imegharimu fedha nyingi sana ili kuwanufaisha wananchi wote kwa kufuata taratibu za kupata huduma hiyo kihalali na si kinyume na taratibu, akisisitiza kuwa ni haki ya mwananchi kupata maji lakini pia ana wajibu wa kuitunza miundombinu ya maji ili itoe huduma ya uhakika na endelevu.

‘‘Ninatangaza vita na wezi wa maji na wahujumu wa miundombinu ya maji, ole wenu wenye tabia hiyo maana tumechoka kwa kuwa inaturudisha sana nyuma kimaendeleo na nitalivalia njuga suala hili mpaka likome’’, amesisitiza Aweso. Aidha, Naibu Waziri Aweso ametembelea mradi wa Hoza Salala uliopo Kijiji cha Kibati, wilayani Mvomero, mradi uliokuwa umegubikwa na tuhuma za ufisadi ambapo ameivunja Bodi ya Maji ya mradi huo na kuagiza iundwe mpya baada ya kugundua matumizi mabaya ya fedha kwa wajumbe wa kamati ya bodi.

Photo: